Date: 
25-05-2023
Reading: 
Zaburi 17:1-8

Alhamisi asubuhi tarehe 25.05.2023

Zaburi 17:1-8

1 Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.

2 Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili.

3 Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,

4 Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.

5 Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.

6 Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu.

7 Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.

8 Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;

Usikie kuomba kwetu;

Asubuhi hii tunamsoma Mfalme Daudi akiomba Bwana asikilize kilio chake. Anaomba apate haki yake, maana amezuia kinywa chake kukosa mbele za Bwana. Daudi anakiri kuacha njia zisizofaa ili kumpendeza Mungu, na anaomba ulinzi wa Bwana milele. Mwisho wa Zaburi hii Daudi anaahidi kumtazama Bwana na kumtegemea kila siku.

Sala ya Daudi inaakisi maisha ya sala kwa Kanisa. Sala inahusu maisha ya kila siku, yaani kumuomba Bwana na kumtazama yeye siku zote. Pia Sala inatuonesha umuhimu wa kuacha njia mbaya kama Daudi anavyoomba. Katika yote, Daudi alitamani kuishi kwa kumtegemea Bwana, lakini alijua ataweza kwa kuomba. Ndiyo maana aliomba kama tulivyosoma. Nasi tuombe siku zote, maana Bwana husikia kuomba kwetu. Amina.

Alhamisi njema.

 

Heri Buberwa