Date: 
19-05-2023
Reading: 
Mwanzo 5:21-24

Ijumaa asubuhi tarehe 19.05.2023

Mwanzo 5:21-24

21 Henoko akaishi miaka sitini na mitano, akamzaa Methusela.

22 Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela miaka mia tatu, akazaa wana, waume na wake.

23 Siku zote za Henoko ni miaka mia tatu na sitini na mitano.

24 Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa.

Ombeni katika jina la Yesu;

Sura ya tano ya kitabu cha Mwanzo ni kitabu cha vizazi vya Adamu. Katika vizazi hivi vya Adamu, somo la asubuhi hii linamuangazia Henoko ambaye katika uzao huu ni kizazi au mtu wa saba;

Yuda 1:14 Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu,

Somo linaonesha kuwa Henoko alienda na pamoja na Mungu katika maisha yake, hadi kuzaa watoto wake wote (22). Mstari wa 24 pia uaonesha Henoko kutembea na Mungu, yaani aliishi kwa kumtegemea Mungu.

Henoko alitwaliwa na Mungu kama mstari wa 24 unavyosomeka. Alitwaliwa na Mungu kwa sababu alimpendeza Mungu;

Waebrania 11:5 Kwa imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.

Henoko alimpendeza Mungu akatwaliwa kutoka duniani. Kumpendeza Mungu ni muhimu kwetu, pale tufanyapo mapenzi yake. Hatuwezi kumpendeza Mungu bila msaada wake, na msaada huu tunaupata kwa kuomba katika jina la Yesu. Sala zetu zinatuweka kwa Bwana, hatimaye kuwa na mwisho mwema. Siku njema.

 

Heri Buberwa