Usharika wa KKKT Kanisa Kuu Azania Front Cathedral tarehe 9 Aprili 2023 ulijumuika na wakristo wote ulimwenguni kusherehekea sikukuu ya Pasaka.
Akizungumza katika ibada ya kwanza iliyofanyika Usharikani hapa, Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa alisema sikukuu ya Pasaka ni muhimu sana katika maisha ya mkristo kwani ni kumbukumbu ya kushinda umauti kwa mwokozi wetu Yesu Kristo.
“Siku ile ya Ijumaa wafuasi wote wa Yesu waliinamisha vichwa vyao chini kwa sababu Mwalimu wao amekufa” alisema Baba Askofu.
"Kufufuka kwa Yesu kunatudhihirishia sisi wakristo wa leo kwamba Yesu Kristo ni Mungu na hakuna linalomshinda, kufufuka kwake kwa vyovyote vile kunaimarisha Imani zetu. Kama Kristo hasingefufuka basi kuhubiri kwetu kungekuwa ni bure, na Imani yetu ni bure na pia tusingekuwa na jambo la kumwelezea kwani angekufa na kutoweka katika ulimwengu huu kama wanadamu wengine."
Wapo watu wengi katika ulimwengu huu wameishi na kufanya mambo makubwa lakini walipokufa hawakurudi tena. Wapo watu wameanzisha dini na hata sasa wana wafuasi wanaowafuata lakini walikufa na hawajarudi tena. Ndugu zangu hatuna Mungu wa kihistoria, tuna Mungu aliye hai,’’ alisema.
Baba Askofu Malasusa pia aliongeza kusema kuwa mtu akifa ndani ya Kristo ni faida na kwamba wote wanaomfuata watapata uzima wa milele. “Kwakuwa Yesu Yu Hai, Na Sisi Tutakuwa Hai” alisisitiza. "Yesu Kristo anatamani siku kama ya leo tunaposherekea Pasaka kila mtu kuanza maisha mapya na kufufuka pamoja naye."
Pia alisema "Kukemea dhambi huwa kuna gharama na wakati mwingine kunaweza kukupunguzia marafiki, lakini dhambi kwako wewe Mkristo ni lazima uikemee. Mkristo umepewa jukumu la kuwa nuru, ili kumulika mahali pote penye giza".
Ibada ya Sikukuu ya Pasaka ilitanguliwa na kipindi cha kwaresma, pamoja na siku ya Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu ambayo ndiyo siku aliyoteswa Yesu msalabani mpaka kufa kwake lakini siku ya tatu ambayo ndiyo Pasaka yenyewe Bwana Yesu alifufuka.
PICHA KUTOKA IBADA ZA PASAKA.
Kutazama Ibada za Pasaka:
Ibada ya Kwanza | Kiswahili: https://www.youtube.com/watch?v=BTXegvKsyBs&t=5813s
Ibada ya Pili | Kiingereza: https://www.youtube.com/watch?v=ZR3z76sIGyk
Ibada ya Tatu | Kiswahili: https://www.youtube.com/watch?v=_SyI-zQD6g0
Ibada ya Jumatatu ya Pasaka | Kiswahili: https://www.youtube.com/watch?v=CTKRKMGs1Ag