Date: 
26-04-2023
Reading: 
Yohana 10:1-6

Hii ni Pasaka 

Jumatano asubuhi tarehe 26.04.2023

Yohana 10:1-6

1 Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi.

2 Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo.

3 Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje.

4 Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.

5 Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.

6 Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.

Yesu Kristo ni Mchungaji mwema;

Katika sura ya 10 ya Injili ya Yohana, Yesu anafundisha juu ya yeye kuwa Mchungaji mwema. Ni baada ya kumponya mtu kipofu (sura ya 9) na maswali kuwa mengi, Yesu akawaambia alikuja ili vipofu waone. Yesu sasa anaendelea kuwaambia kuwa amwaminiye lazima akae zizini.Asiyekaa zizini siyo kondoo, ni mwizi na mnyang'anyi! Yesu anasisitiza kondoo kuisikia sauti ya Mchungaji na kukaa zizini. Hawakumwelewa, ndipo Yesu akazidi kuwaambia;

Yohana 10:11 Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.

Yesu alipofundisha kuwa yeye ni Mchungaji mwema, na kondoo wakae zizini alimaanisha kuwa yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu, na watu wote wanatakiwa kumwamini na kumpokea yeye. Wema wake hauchagui. Sisi sote tunaalikwa kukaa zizini, yaani kukaa na Yesu siku zote za maisha yetu ili atubariki maishani na kutupa uzima wa milele. Amina.

Uwe na Jumatano njema.

 

Heri Buberwa 

Mlutheri