Hii ni Pasaka
Ijumaa asubuhi tarehe 21.04.2023
Danieli 2:25-30
25 Ndipo Arioko akamwingiza Danielii mbele ya mfalme kwa haraka, akamwambia hivi, Nimemwona mtu wa hao wana wa Yuda waliohamishwa, atakayemjulisha mfalme ile tafsiri.
26 Mfalme akajibu, akamwambia Danielii, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake.
27 Danielii akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu;
28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi;
29 Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa.
30 Lakini mimi, sikufunuliwa siri hii kwa sababu ya hekima iwayo yote niliyo nayo zaidi ya watu wengine walio hai, bali kusudi mfalme afunuliwe ile tafsiri, nawe upate kujua mawazo ya moyo wako.
Yesu Kristo ajifunua kwa wanafunzi wake;
Jumatatu asubuhi tuliona jinsi Mfalme Nebuchadnezzar alivyoota ndoto, na hakuna aliyeweza kuitafsiri ndoto ile. Baada ya waganga, wachawi na wenye hekima kushindwa kutafsiri ndoto, mfalme aliamuru wote wauawe. Ndipo akatafutwa Danieli kutafsiri ndoto, akawaambia wenzake waombe rehema ya Mungu ili tafsiri ya ndoto ipatikane.
Katika somo letu asubuhi hii tunamuona Danieli akiwa mbele ya mfalme, anamwambia ni Mungu pekee awezaye kufunua siri. Kwa maana nyingine anamwambia kwamba ni Mungu pekee awezaye kutafsiri ndoto. Daniel aliitafsiri ndoto ya mfalme, hadi mfalme akamsujudia Danieli.
Danieli anaonesha uwezo wa Mungu aliyemwezesha kutafsiri ndoto. Kumbe hapa anatupa funzo kuwa maisha yetu yatakuwa magumu tusipomtegemea Bwana, maana hatutapata suluhisho la kujua tuishi vipi katika Kristo. Kama Mungu alivyomwezesha Danieli kutafsiri ndoto, Yesu anajifunua kwetu kama Mwokozi wetu, atuwezeshaye katika yote. Dumu katika imani ukimwamini yeye, sasa na hata milele. Amina.
Nakutakia Ijumaa tulivu.
Heri Buberwa