Date:
13-10-2022
Reading:
Wagalatia 5:7-12
Alhamisi asubuhi tarehe 13.10.2022
Wagalatia 5:7-12
[7]Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli?
[8]Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi.
[9]Chachu kidogo huchachua donge zima.
[10]Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote.
[11]Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika!
[12]Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!
Kristo ametuweka huru;
Watu wa Galatia waliipokea Injili vizuri tu, lakini baadaye wakaanza kupita walimu waliofundisha uongo. Walimhubiri Kristo wakikazia sheria! Lakini katika somo la leo asubuhi Mtume Paulo anawasihi Wagalatia kutoshawishiwa na mafundisho ya uongo wakiitii kweli. Paulo anakazia kuwa wako huru toka dhambini pale anaposema;
Wagalatia 5:13 [13]Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.Somo la asubuhi hii linatukumbusha kutoshawishiwa na mafundisho ya uongo yaliyoshamiri kwa sasa. Tutambue kuwa Yesu Kristo ametukomboa kwa kutufia msalabani. Walimu wa uongo siyo tu tuwakatae, bali tuwakemee ili wasiliharibu Kanisa la Kristo. Tunawajibika kuifundisha kweli ili jamii yote ifahamu kuwa Kristo ametuweka huru. Tuko huru toka dhambini. Siku njema.