Event Date: 
12-08-2022

Kamati ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Usharika wa KKKT Kanisa Kuu Azania Front Cathedral hivi karibuni (Juni 25, 2022) iliandaa kambi ya matibabu (Afya Check) kwa ajili ya kupima na kutoa huduma za kitabibu kwa washarika na wananchi wote.

Kambi hiyo ya siku moja ilifanyika katika viwanja vya Usharika wa Azania Front ambapo zaidi ya wananchi 400 walihudhuria kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Samuel Swai, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi waliofika kupata huduma za kitabibu walikuwa ni washarika wa Azania Front. Katika kambi hiyo huduma za vipimo na ushauri wa kitaalam zilipata kutolewa huku waliobainika kuwa na changamoto mbalimbali za kiafya wakianza utaratibu wa kupata tiba.

Baadhi ya vipimo vilivyotolewa ni pamoja na Kifua Kikuu (TB), Matatizo ya Macho, Matatizo ya Mifupa, Changamoto za Kiakili na vipimo vingine kadhaa. Pia zoezi la kuchangia damu lilifanyika ambapo washarika na wananchi mbalimbali walipata fursa ya kuchangia damu kwenye Benki ya Taifa ya Damu Salama.

Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dk. Alex Malasusa aliwapongeza washarika kwa kujitokeza kwa wingi kuchunguza na kupata majawabu mbalimbali kuhusu afya zao. Pia aliwashukuru madaktari na wauguzi wote waliojitolea kusimamia zoezi hilo ambalo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Nawasihi washarika waliopimwa na kukutwa na changamoto mbalimbali za kiafya kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalam wetu, na wale walioambiwa waende mbele zaidi kuwaona wataalam hospitalini naomba mfanye hivyo na Mungu atawaponya,” alisema Baba Askofu.

----------------------

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kambi ya matibabu iliyofanyika katika viwanja vya Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral.