Date: 
28-02-2022
Reading: 
Mathayo 20:20-23

Jumatatu asubuhi tarehe 28.02.2022

Mathayo 20:20-23

20 Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno.

21 Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.

22 Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.

23 Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

Tazameni tunapanda kwenda Yerusalemu;

Sura ya 20, inaanza na mfano wa mkulima aliyeajiri watu shambani. Walianza kwa muda tofauti toka asubuni, lakini wote wakalipwa malipo sawa. Walioanza asubuhi walilalamikia kulipwa sawa na walioanza jioni, lakini mwenye shamba aliwaambia kuwa alikuwa na haki ya kutumia mali yake apendavyo, na kubwa zaidi, walipatana dinari! Kwa sehemu hii, Yesu anatufundisha kuwa wote tuko sawa mbele zake (zingatia hili).

Baadaye Yesu anatoa taarifa ya tatu ya kukamatwa na kufa kwake (somo la mahubiri la jana)

Sasa tunapokuja somo la leo asubuhi, tunamuona mama yao Yakobo na Yohana akiomba kwa Yesu wanae wakae mmoja kulia kwake na mwingine kushoto, katika Utukufu wake.

Ukisoma Injili ya Marko, inaonekana Yakobo na Yohana ndio wanaongea na siyo mama yao;

Marko 10:35-37

35 Na Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba.
36 Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini?
37 Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.

Jambo muhimu hapa ni kuwa wote watatu, yaani Yakobo, Yohana na mama yao walikuwa na nia moja tu, Yohana na Yakobo kukaa mmoja kulia na mwingine kushoto kwa Yesu.

Hawa ndugu walitaka nafasi ya heshima kuliko wenzao, ndio maana ukiendelea kusoma, wenzao waliwakasirikia!

Mathayo 20:24 Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili.

Hapo juu kwenye mfano wa mkulima na watendakazi wake, tumeona kuwa wote walilipwa dinari, kuonesha kwamba sote tuko sawa mbele za Mungu. Kwa muda mfupi tu, Yakobo na Yohana walianza kuomba nafasi ya heshima, badala ya kuomba njia ya kuingia mbinguni!

Maisha na sala zetu yaakisi mambo mema mbele za Mungu ambayo yanatuongoza kuurithi uzima wa milele, na siyo maisha ya dhambi yaliyojaa ubinafsi kama wa Yakobo na Yohana. Tumia fursa vizuri mbele ya Yesu, pale unapoomba akuongoze, ili akupe maisha mazuri, yenye mwisho mwema.

Nakutakia maandalizi mema ya Kwaresma.