JUMATATU TAREHE 15 NOVEMBA 2021
Amosi 9:1-6
1 Nalimwona Bwana akisimama karibu na madhabahu; akasema, vipigo vichwa vya nguzo, hata vizingiti vitikisike; vivunje vipande vipande juu ya kichwa cha kila mmoja wao; nami nitamwua mtu wa mwisho wao kwa upanga; hapana hata mmoja wao atakayekimbia, wala hataokoka hata mmoja wao.
2 Wajapochimba waingie katika kuzimu, mkono wangu utawatoa huko; nao wajapopanda hata mbinguni, nitawatelemsha toka huko.
3 Nao wajapojificha katika kilele cha Karmeli, nitawatafuta na kuwatoa toka huko; na wajapositirika katika vilindi vya bahari nisiwaone, nitamwagiza joka huko, naye atawauma.
4 Nao wajapokwenda hali ya kufungwa mbele ya adui zao, nitauagiza upanga huko, nao utawaua; nami nitawaelekezea macho yangu niwatende mabaya, wala si mema.
5 Kwa maana Bwana, MUNGU wa majeshi, ndiye aigusaye nchi, nayo ikayeyuka, na wote wakaao ndani yake wataomboleza; nayo itainuka yote pia kama Mto, nayo itakupwa tena kama Mto wa Misri.
6 Yeye ndiye avijengaye vyumba vyake mbinguni, na kuweka misingi ya kuba yake juu ya nchi; yeye ndiye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA ndilo jina lake.
Hukumu ya mwisho;
Amosi alitoa unabii wake wakati wa utawala ya Yeroboamu wa pili wa Israeli na mfalme Uzia wa Yuda. Zilikuwa ni nyakati za kilele cha maendeleo na mafanikio. Kulikuwa na mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi, kutoka kilimo na ufugaji, na kuegemea kwa wafanyakazi na biashara. Maskini na wasiokuwa na uwezo waliongezeka na kunyanyaswa. Magendo na rushwa vilishamiri.
Amosi aliikemea hali hiyo, akitoa ujumbe wa kutenda haki kama Mungu alivyo wa haki. Aliwatetea maskini na kuwashutumu hadharani wafanyabiashara wadanganyifu wenye dhuluma na jeuri, na viongozi wavunja sheria, wala rushwa.
Mungu alimtuma nabii Amosi alete ujumbe wa toba.
Ujumbe wa leo asubuhi ni kuangamizwa kwa Israeli, kama wangeendelea na tabia za kukandamiza wanyonge, kuendekeza vitendo vya rushwa na unyanyasaji.
Tunapewa ujumbe wa kujenga jamii yenye kutenda haki, kukemea vitendo viovu, ikiwemo unyanyasaji kwa watu wanyonge. Tusijenge jamii yenye matabaka, ambapo wachache wanafurahia maisha na wengi kuumia. Mwisho wa uovu wote huo ni hukumu ya kwenda kwenye ziwa la moto. Ni wajibu wa Kanisa kujenga jamii yenye haki kwa kukemea uovu, ili asiwepo hata mmoja wa kuukosa ufalme wa Mungu, pale Yesu atakaporudi kulichukua Kanisa.
Uwe na wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.