Event Date: 
31-03-2021

Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, Mchungaji Charles Mzinga mnamo tarehe 1 Agosti 2020 alifanya uzinduzi wa klabu ya vijana ya usomaji na kujifunza biblia ijulikanayo kama Azaniafront Youth Bible Club (AYBC). Kuanzishwa kwa klabu hiyo kunalenga kuwapa fursa vijana wa Azaniafront kusoma, kuchambua, kujadiliana na kujifunza biblia kwa kina.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa klabu hiyo iliyofanyika usharikani Azanifront, Mchungaji Mzinga aliwaambia vijana kutumia fursa ya kuwepo kwenye klabu hiyo kwa kujifunza neno la Mungu ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa Kristo Yesu katika jamii zao. “Mnapokuwa mnakutana hapa kwa ajili ya kujifunza neno la Mungu kupitia klabu hii maalum kwa vijana, ni matumaini yangu kuwa mtazingatia na kuyaishi mafundisho mnayoyapata ili muweze kuwa mfano wa kuigwa na vijana wengine,” alisema Mchungaji Mzinga.

Akizungumza juu ya vigezo na masharti ya kujiunga na klabu hiyo ambayo hukutana kila siku za Jumatano saa 11 jioni, Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Oneska James, alisema ili kijana aweze kujiunga na AYBC lazima awe tayari amepata kipaimara, awe na nia ya dhati ya kutaka kujifunza neno la Mungu na pia awe na utayari wa kusaidia vijana wenzake kulifahamu neno la Mungu.

Kwa mujibu wa Oneskas, klabu ina mpango wa kupanua wigo na kuwafikia vijana wengi kadri inavyowezekana ili kuhakikisha neno la Mungu linawafikia vijana wote. “Napenda kuwakaribisha vijana wote wa Azaniafront wanaokidhi vigezo vya kujiunga na klabu yetu kufanya hivyo ili tuweze kujifunza neno la Mungu pamoja kwani hii ni fursa adimu ambayo itatusaidia kuyajua vizuri maandiko na hivyo kutuimarisha kiimani na kiroho,” Oneska alieleza.