Date: 
10-02-2023
Reading: 
Mathayo 20:1-16

Ijumaa asubuhi tarehe 10.02.2023

Mathayo 20:1-16

1 Kwa maana ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu.

2 Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu.

3 Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;

4 na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda.

5 Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile.

6 Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?

7 Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.

8 Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza.

9 Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.

10 Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.

11 Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba,

12 wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.

13 Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?

14 Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15 Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?

16 Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.

Tunaokolewa kwa neema;

Yesu anatoa mfano wa mwenye shamba ambaye aliwapa watu kazi kwa muda tofauti, lakini akawapa malipo kwa ngazi moja. Haikuwa rahisi kwake, maana walioanza kazi mapema walitegemea malipo makubwa kuliko walioanza kwa kuchelewa, lakini mwenye shamba aliwalipa wote walichopatana.

Mfano huu unaonesha Yesu asivyo na upendeleo. Watu wote ni sawa mbele zake, na ndiyo maana alivyokuja duniani alitoa huduma kwa watu wote. Kwa hiyo sisi sote tunaalikwa kumpokea huyu Yesu aliyekufa kwa ajili ya wote, ili atuokoe na hatimaye kutupa uzima wa milele. Milango i wazi, mwamini Yesu uokolewe.

Ijumaa njema.

Heri Buberwa