Date: 
20-02-2023
Reading: 
Mathayo 16:13-16

Jumatatu asubuhi tarehe 20.01.2023

Mathayo 16:13-16

13 Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?

14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.

15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

Tazameni tunapanda kwenda Yerusalemu;

Sura ya 15 ya injili ya Mathayo tunasoma Yesu akilisha watu elfu nne kwa mikate saba na samaki wachache. Katika sura ya 16 Mafarisayo na Masadukayo wanamuomba Yesu awaoneshe ishara itokayo mbinguni. Yesu anawaita wanafiki! Aliachana nao akaondoka, akaenda na wanafunzi wake ng'ambo. 

Huko ng'ambo Yesu akawaambia wanafunzi kuwa makini na chachu ya Mafarisayo, yaani kuepuka mafundisho yao.

Ndipo katika somo la leo asubuhi hii, baada ya ishara na mafundisho yote anawauliza wanafunzi wake kuwa watu husema yeye ni nani? Alipewa majibu kadhaa, lakini Simoni Petro alimwambia kwamba yeye (Yesu) ni Kristo, mwana wa Mungu aliye hai.

Simon Petro alitambua na kusema moja kwa moja kuwa Yesu ndiye Kristo. Yesu Kristo ndiye mwokozi wa ulimwengu, aliyeiendea njia ya mateso kwa ajili ya wokovu wetu. Aliteswa yeye, sisi tuokolewe. Yesu anapopanda kwenda Yerusalemu ni tangazo la kuelekea kufa ili atuokoe. Tudumu katika Kristo aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu.

Nakutakia wiki njema yenye ushuhuda.

Heri Buberwa