Hii ni Kwaresma
Jumamosi asubuhi tarehe 02.04.2022
Mathayo 15:32-39
32 Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani.
33 Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii?
34 Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache.
35 Akawaagiza mkutano waketi chini;
36 akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano.
37 Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa.
38 Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila wanawake na watoto.
39 Akawaaga makutano, akapanda chomboni, akaenda pande za Magadani.
Yesu ni mkate wa uzima;
Jumatatu asubuhi tuliona Yesu akiwalisha watu elfu tano. Jumamosi ya leo tunaona Yesu akiwalisha watu elfu nne.
Yesu hakufanya ishara mpya kuwalisha watu elfu nne, na hakuwa amepanga kufanya hivyo. Alichofanya ni kuwahudumia watu aliokuwa nao, akiunganisha tukio hili na maandiko matakatifu, kuwa Mungu anawajali watu wake.
Katika somo hili tunaona yafuatayo;
1. Huruma ya Yesu
Yesu anadhihirisha kuwa yeye ni mwenye huruma. Watu aliokuwa nao kwa siku tatu anaona bora kwanza wale ndio waondoke. Mpaka inafikia hatua hii, inawezekana;
-Labda kuna waliomfuata kumuomba chakula
-Labda eneo lenyewe lilikuwa halina chakula, maana ilikuwa nyika
-Labda kuna waliomlilia njaa
- Labda aliona wamechoka na hawawezi kurudi nyumba ni kwao n.k
Vyovyote vile, hapa tunajifunza kuwa Yesu ni mwenye huruma. Tunapoendelea na tafakari ya majira haya, tunakumbushwa kumwendea Yesu mwenye huruma, lakini nasi pia kuwa na huruma kwa wenzetu. Huruma ianzie kwetu. Haiwezekani tukose huruma, halafu tuombe huruma. Tuishi kwa kuhurumiana, ndipo Taifa la Mungu litastawi.
2. Utoaji wa Yesu
Yesu alijua watu wana njaa, na alijua ana uwezo wa kuwapa chakula, akawapa.
Yaani alitoa alichokuwa nacho.
Kwa kifupi tu, wewe unatoa ulicho nacho kuwasaidia wengine?
3. Yesu anatosha.
Yesu anatoa chakula na walaji wanasaza. Wanafunzi waliogopa hata watu wasubiri kula, lakini Yesu anawapa chakula na wanasaza. Wanafunzi walitumia akili zao kuwa chakula hakipo! Kumbe hawakujua kuwa hawakujitosheleza, ila Yesu angetosha.
Wanafunzi walichotakiwa kujua ni kuwa katika huduma yao walitakiwa kumtegemea Yesu ili kuutimiza utume wao. Kitendo cha wanafunzi kuuliza watu watakula nini, ni dhahiri waliamini hawawezi kuwahudumia wale watu. Hawakukumbuka kuwa Yesu hashindwi lolote.
Katika maisha yetu, tunahitaji Yesu atuongoze ili tuweze kuifanya kazi yake. Haiwezekani kazi ya Mungu tukaifanya kwa nguvu zetu wenyewe. Bila Yesu hatujitoshelezi!
Ndio maana tunaambiwa kuwa Yesu ni mkate wa uzima.
Ndugu yangu;
Yesu ndiye chakula kilichoshuka kutoka juu kwa ajili ya wanadamu wote. Mwamini Yesu aliye chakula cha uzima, ili uupate huo uzima.