Hii ni Pasaka;
Jumanne asubuhi tarehe 19.04.2022
Matendo ya Mitume 13:16-25
16 Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni.
17 Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza.
18 Na kwa muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa.
19 Na alipokwisha kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini;
20 baada ya hayo akawapa waamuzi hata zamani za nabii Samweli.
21 Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini.
22 Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.
23 Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;
24 Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake.
25 Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.
Tembea na Yesu mfufuka;
Mtume Paulo anahubiri akitoa historia ya ukombozi wa Israeli, jinsi walivyokombolewa toka utumwani. Anaeleza kuwa ni katika uzao huo wa Israeli walitokea watawala mbalimbali akimtaja Daudi mwana wa Yese. Ni katika uzao huo huo alitokea Yesu Kristo.
Paulo anachoonesha hapa ni mpango wa Mungu wa wokovu tangu kale. Kwamba aliwakomboa wanadamu kwa kila hatua, baadaye akaja Yesu aliyejitoa msalabani mara moja, ili kuukomboa ulimwengu.
Yesu huyu ndiye aliyeteswa, akafa, akazikwa, na siku ya tatu akafufuka kwa ajili yetu. Hivyo mazingira ya wokovu yalikwisha kuwekwa tayari. Tunawajibika kumpa Yesu maisha yetu, ili tudumu katika wokovu. Yaani tutembee na Yesu mfufuka.
Siku njema.