Jumamosi asubuhi tarehe 27.11.2021
Marko 12:18-27
[18]Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema,
[19]Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao.
[20]Basi kulikuwa na ndugu saba, wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao.
[21]Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika;
[22]hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.
[23]Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.
[24]Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?
[25]Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni.
[26]Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?
[27]Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.
Uzima wa Ulimwengu ujao;
Masadukayo wanamuuliza Yesu, kuhusu mwanamke aliyeolewa na ndugu saba bila uzao, kuwa siku ya ufufuko atakuwa mke wa nani? Yesu anajibu kuwa kwa ufufuko hakuna habari ya kuoa wala kuolewa.
Tuwaze yapasayo utukufu wa Mungu na uzima wetu, na siyo kuwaza yasiyotusaidia katika kuuendea uzima wa milele. Tukiwaza isivyostahili tunapotea. Mawazo yetu yatuongoze kutenda mema ili tuurithi uzima wa milele.
Siku njema.