Date: 
19-09-2022
Reading: 
Marko 12:13-17

Jumatatu asubuhi tarehe 19.09.2022

Marko 12:13-17

[13]

Wakatuma kwake baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno.

[14]Hata walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo?

[15]Tumpe, tusimpe? Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione.

[16]Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari.

[17]Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana.

Uwakili wetu kwa Mungu;

Mafarisayo na waandishi walitumia kila njia kuonesha kwamba Yesu hakuwa sahihi katika mafundisho yake. Maswali waliyomuuliza yalilenga kuonesha kwamba hakuwa sahihi. Leo asubuhi tunasoma baadhi ya wakuu na Mafarisayo wakimuuliza Yesu juu ya kulipa kodi. Naye anawaambia wampe Kaisari ya kwake, na Mungu wampe yaliyo yake.

Tunapofanya kazi zetu sharti tuwajibike kwa mamlaka husika hapa duniani, yaani tumpe Kaisari yaliyo yake. Lakini tufahamu ya kuwa vyote tulivyo navyo ni mali ya Mungu, hivyo tusiache kumtolea kwa ajili ya kazi yake. Tunawajibika kumtolea Mungu, maana sisi tu watunzaji tu wa mali zake, hivyo tunapomtolea tunampa vilivyo vyake.

Nakutakia juma lenye uwakili mwema.