Date: 
14-04-2022
Reading: 
Luka 22:14-20

Hii ni Alhamisi Takatifu;
Alhamisi ya tarehe 14.04.2022
Siku ya kuwekwa Chakula cha Bwana;

Masomo;
Zab 116:5-9
1Kor 11:29-34
*Luka 22:14-20

Luka 22:14-20
14 Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye.
15 Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu;
16 kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.
17 Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi;
18 Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja.
19 Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
20 Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]

Agano jipya katika Mwili na Damu ya Yesu;

Hata saa ilipofika (14)
Luka anatumia maneno "hata saa ilipofika...." hii huaķisi ukuu  wa Mungu, kwamba ilipofika saa ya kumkomboa mwanadamu, Mungu alikuwa amekwisha kuandaa kila kitu, tayari kwa ukombozi. Hakuna lililotokea hadi muda ulipofika. Yesu alilijua hili.

Kwa mtiririko toka Injili ya Yohana;
-Mwanzoni kabisa mwa huduma yake, Yesu alimwambia Maria mama yake kuwa saa yake ilikuwa haijawadia (Yoh 2:4)
-Baadaye akiongea na ndugu zake kuhusu sherehe/tamasha la kiyahudi aliwaambia "saa yangu haijawadia mimi kuondoka...." (Yoh 7:6:8)
-Yesu alipokuwa akiongea na wanafunzi wake kuhusu kifo chake, alisema "sasa wakati umewadia wa Mwana wa Adamu kuingia katika utukufu wake... (Yoh 12:23)
-Tena, alipokaribia kusulubishwa ukuu wa Mungu ulikuwa wazi. Yohana anaadika "kabla ya kusherehekea Pasaka, Yesu hali alijua saa imefika ya kurudi kwa Baba yake..." (Yoh 13:1)
-Kukamatwa na kusulubiwa kwa Yesu kulipokaribia, Yohana  anaandika sala ya Yesu "Yametimia umtukuze mwanao..."

Wayahudi hawakuweza kumdhibiti Yesu hata walipomkamata, walipompiga, wakamwamba msalabani na kumfanyia dhihaka. Utukufu wa Mungu ulionekana katika kusulibishwa kwake. Kilichotokea ndicho kilichotakiwa kwa mpango wa Mungu wa wokovu kukamilika.

Yako mazingira na wakati wa maumivu maishani mwetu. Ipo milima na mabonde ya kupita. Lakini tunao uwezo wa kuvuka mazingira hayo kwa kujiamini tukijua ya kuwa Mungu ndiye mdhibiti wa hali zote. Hivyo unaposhiriki karamu takatifu leo, fahamu ya kuwa Mungu ni wa utukufu, mdhibiti wa vitu vyote.

Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; (15)
Ni kwa nini Yesu alitamani kuila Pasaka pamoja na wanafunzi wake kabla ya mateso yake?
-Huu ulikuwa muda wake wa mwisho akiwa nao.
-Yesu alikuwa akionesha alivyopenda ushirika na waaminio, akiwafundisha kukaa pamoja.
-Alikuwa akiibadili sherehe ya Pasaka kuwa karamu takatifu. Ulikuwa ni wakati wa kubadili Pasaka ya Agano la kale iliyohusisha kumwagwa kwa damu ya mwana kondoo na kuwa karamu takatifu ya Agano jipya, ambayo ingehusisha damu yake (Luka 22:20)
Yesu hapa anatukumbusha kuwa tunashiriki mwili na  damu yake ya Agano jipya kwa ondoleo la dhambi kuelekea uzima wa milele

Akapokea kikombe akashukuru  (17)
Mstari wa 17 unaonesha Yesu akitwaa kikombe cha mvinyo na kushukuru na kuwaambia twaeni mgawane ninyi kwa ninyi.

Inaaminika wakati wa Pasaka kulikuwa na vikombe tofauti vinne vilivyokuwa na maana tofauti (Jeff Stott)
Luka anataja vikombe viwili  kikombe cha baraka(17), na  cha neema(20). Yesu anapotoa kikombe, anatufanya kutafakari kuwa;
-Kikombe cha baraka na neema  huonesha ushirika wa waaminio. Kwa pamoja sote tunaipata neema itokayo kwa Mungu yule yule, msamaha mmoja toka kwa Mungu yuleyule, sote tumekuwa viumbe vipya, na tunakunywa kikombe kimoja. Japokuwa wapo wanaoweza kuwa tofauti (kama Yuda aliyekuwa mezani) lakini lengo la Yesu ni kutukumbusha ushirika wetu katika imani,kuliko mgawanyiko.
-Yesu anatukumbusha kuwa wenye shukrani. Tunaishi katika dunia ambayo imejaa ulinganifu, kutoshukuru na kutambua neema ya Mungu. Tunakumbushwa kushukuru. Yesu alitwaa kikombe akashukuru.
Mojawapo ya ushuhuda wa mkristo aliyekomaa ni shukrani kama Mtume Paulo anavyowaasa Wakolosai;
Wakolosai 2:6-7
6 Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye;
7 wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani.

Kuwa mtu wa shukrani. 
Kunywa kwenye kikombe cha baraka.

Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega (19)
Katika injili hii hii ya Yohana, Yesu alijieleza tofauti kulingana na mazingira ili kueleweka. Mfano, Yesu anajiita mlango (10:9), anajiita mzabibu (15:5) kutaja hivyo tu. Leo Yesu anawapa wanafunzi mkate na kusema "huu ni mwili wangu uliotolewa kwa ajili yenu..."
Kumbuka ilikuwa Pasaka, na mkate hapa ulitengenezwa maalumu kwa ajili ya Pasaka. Mkate huu bila shaka ulipitia hatua zote za kupikwa kama kukanda unga, kuokwa, mvuke kutumika n.k  
Yesu anatutaka kujenga picha ya jinsi mkate unavyopitia hatua ngumu hadi kuwa tayari kuliwa,kuwa  ndivyo hivyo aliteseka msalabani hadi kufa kwa ajili yetu. Hivyo anatuita kukumbuka mateso yake kwa ajili ya wokovu wetu.

Hitimisho;
Yesu ndiye mwana kondoo wa Pasaka aliyejitoa msalabani mara moja, akitoa mwili wake na damu yake kwa ajili yetu. Anatualika kushiriki meza takatifu kwa ajili ya ondoleo la dhambi. 
Nakuacha na swali;
Unashiriki kwa haki?
Au unajitafutia hukumu?
Njooni tule karamuni.