Date: 
28-10-2022
Reading: 
Luka 17:11-19

Ijumaa asubuhi tarehe 28.10.2022

Luka 17:11-19

[11]Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya.

[12]Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,

[13]wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!

[14]Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.

[15]Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu;

[16]akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria.

[17]Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?

[18]Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu?

[19]Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.

Imani yako imekuponya;

Yesu anapita katikati ya Samaria na Galilaya, huko anakutana na kundi la watu kumi wenye ukoma. Inawezekana walikuwa wamekwisha kusikia habari zake, maana walipomuona walipaza sauti wakisema;

Luka 17:13

[13]wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!

Yesu aliwaambia wakajioneshe kwa makuhani, wakiwa njiani wakatakasika. Kwa nini aliwaambia wakajioneshe kwa makuhani?

-Wale makuhani ndiyo waliowafahamu, maana waliabudu huko. Hivyo kupona kwao kungekuwa dhahiri tofauti na sasa ambapo mtu anaweza kudai kupona wakati hapo kwenye eneo la tukio hakuna anayemfahamu. Unakuta mkutano uko Tanga, mhubiri katoka Arusha, aliyepona katoka Iringa. Hakuna wa kuthibitisha uponyaji.

-Yesu alitaka wakiisha kutakasika wakatoe sadaka huko huko walikoabudu. Siyo siku hizi ambapo sadaka inakuwa lazima unapokuwa, tena kwa vitisho! 

Wakati mwingine unalazimishwa utoe ili uombewe! Yesu aliwaponya akawaruhusu kuondoka. Haimaanishi tusitoe sadaka, bali kwa utaratibu, lakini Imani yako kwa Mungu ikuongoze kutoa kwa ajili ya kazi yake.

Walioponywa ni kumi, ila alirudi mmoja kushukuru. 

Sisi tuwe na shukrani. Tukiisha kupokea haja zetu tukumbuke kumshukuru Mungu.

Wenye ukoma walimuita Yesu akawatakasa.

Nasi tukimuita kwa Imani, Yesu hutupa haja zetu.

Ijumaa njema