Date:
24-12-2021
Reading:
Isaya 9:2-3
Hii ni Noeli;
Usiku Mtakatifu, Tarehe 24.12.2021
Masomo;
Zab 108
Rum 8:31-35
*Isa 9:2-3
Isaya 9:2-3
2 Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. 3 Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara.
Yesu amezaliwa kwa ajili yetu;
Haleluya.
Sura za 7 na 8 za kitabu cha Isaya zinaeleza habari ya mfalme Ahazi, pale mfalme Rezini wa Shamu na mfalme Peka walipoungana kupigana na Israeli (7:1). Isaya alimsihi Ahazi kutowaogopa Rezini na Peka (7:3-4) kwa sababu Mungu angeikomboa Yerusalemu. Ahazi hakuamini, akatuma ujumbe kwa mfalme Tiglath-pileseri wa Ashuru akiomba msaada kuwakabili Rezini na Peka (2Fal16:7). Ahazi alichukua vifaa vya thamani hekaluni akavituma kwa mfalme Tiglat, akaanza ibada za waAshuru (2Fal16:10)
Inakadiriwa kuwa mfalme Tiglat alifanya alivyoombwa na mfalme Ahazi mwaka 733 hadi 732KK akiwashinda Israeli na kuwafanya mateka. Huu ni wakati uliopita unaotajwa katika mstari wa kwanza wa sura ya 9
Isaya 9:1 Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa.Pia ni wakati wa giza kama ulivyotajwa katika mstari wa pili (angalia juu kabisa kwenye somo la leo). Ulikuwa ni wakati kabla ya uhamisho. Ni giza lililoletwa na uongozi wa mfalme Ahazi, kwa kutomwamini Mungu, kisha kujiunga na Tiglath-pileseri.
Ndipo ujumbe wa leo unaonesha kuwa Mungu bado hakuwaacha Yerusalemu. Ni dhahiri hata leo katika zama hizi tunazoishi, kila mmoja wetu anaweza kuwa yuko gizani. Yaani lipo jambo lako haliendi vizuri, na wakati mwingine huenda umekata tamaa.
Mungu hajawahi kukuacha.
Mungu hajakuacha.
Mungu hatakuacha.
Tuendelee na uchambuzi;
Katika mpango wa Mungu wa wokovu kwa Taifa lake, Isaya alimwambia Ahazi habari ya bikira kupata mimba na kuzaa mtoto mwanamume, atakayeitwa Immanuel;
Isaya 7:14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.Ahadi hii inajirudia katika sura ya 9:6, hivyo kuonesha kuwa Mungu alikuwa na Yerusalemu. Mungu aliahidi kuwa giza walilokuwamo halingekuwa mwisho wao, kwa sababu Bwana angewakomboa.
Zabuloni na Naftali (wanatajwa 9:1) walikuwa miongoni mwa makabila 12 ya Israeli na walikuwa karibu na bahari ya Galilaya eneo ambalo wakati wa Yesu lilikuwa sehemu ya huduma yake. Watu wa Zabuloni na Naftali kwa sababu ya kuwa Kaskazini mwa Israeli walikuwa wa kwanza kuwa chini ya Ashuru, lakini inatabiriwa kuwa wangekuwa wa kwanza kuiona kazi ya Mesiya.
Katika Agano jipya, tunasoma unabii wa Isaya ukikamilika;
Mathayo 4:13-16
13 akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali; 14 ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, 15 Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, 16 Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia.Maeneo yaliyokaliwa na mfalme Tiglath-pileseri yalitabiriwa kuwa ya kwanza kumwona Bwana. Ni kama sisi ambavyo tutamwona Bwana, pamoja na magumu yote tunayopitia.
Giza huambatana na mambo mengi. Katika giza mtu huenda polepole, kwa tahadhari. Mara nyingi huwa tunakuwa waoga kwenye giza kwa sababu hatuwezi kuona vizuri, wala hatujui kuna nini. Tunalala usiku tena kwa sala, lakini kwa sababu kuna giza tunafunga milango na madirisha.Katika maisha ya imani, giza linahusishwa na hali ya kuwa mbali na uso wa Bwana. Pale mtu asipomjua Kristo anakuwa gizani. Lakini zaidi, ni pale maisha yetu yanapokuwa hayampi Mungu utukufu, yaani matendo, mawazo na maneno yetu hayamtukuzi Mungu. Tunapokuwa dhambini tunakuwa gizani. Yesu alileta nuru, lakini alihuzunika kwa waliomkataa;
Yohana 3:19-2119 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. 20 Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. 21 Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.Yesu alikuja kututoa gizani, alileta nuru. Giza ni dhambi tulizomo. Tunaitwa kutoka. Tunatoka gizani na kuingia nuruni kwa kufanya toba, ambapo kwa neema tunatangaziwa msamaha wa dhambi na Yesu Kristo aliyezaliwa.
Tunapokumbuka kuzaliwa kwa Yesu usiku huu, tumpe mioyo yetu kwa kulikataa giza, yaani dhambi. Ujio wa Yesu ni kwa ajili ya wokovu kwa wote. Umempokea?
Tubu dhambi
Toka gizani
Ingia nuruni.
Nakutakia ibada njema ya usiku Mtakatifu.