Hii ni Kwaresma;
Jumatano ya tarehe 02.03.2022
Siku ya majivu;
Masomo;
Zab 85:8-13
Mt 9:9-13
*Isa 58:6-9
Isaya 58:6-9
6 Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?
7 Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?
8 Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.
9 Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;
Kutubu na kurejea kwa Bwana;
Jumapili iliyopita, tuliongozwa na tafakari ilisema "Tazameni tunapanda kwenda Yerusalem", taarifa aliyoitoa Yesu akielezea hatima yake aliyokuwa akiifahamu. Hatma yake hiyo iliambatana na mateso makali, ambapo ilifikia hatua ya kuomba kikombe kimuepuke. Ujumbe mkubwa hapa ni kuwa Yesu aliiendea njia ya mateso, ambayo tunapata nafasi ya kuyatafakari wakati huu, kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Hivyo, mwanadamu hana budi kuishi maisha ya toba wakati wote, ili kuuishi wokovu huu ambao Yesu ametupa kwa njia ya mateso.
Hiki ni kipindi cha kutafakari juu ya maisha yetu. Tunaitwa kutafakari njia zetu, na tunakumbushwa kuwa, tunatakiwa kuishi maisha ya Imani, toba na msamaha siku zote. Majira haya yamewekwa kutukumbusha tu, sio kwamba tutende mema tu kipindi hiki, la hasha!
Tukirudi kwenye Somo;
Baada ya kutoka uhamishoni, wayahudi walipotoka Babeli, wakakaa katika nchi yao, walianza kujiuliza maswali kuhusu matazamio yao. Nabii Isaya anawapa moyo na kuwapa matumaini ya hali njema hapo baadae. Mojawapo ya njia ya kuwa na matumaini mema, ni kuwa na ibada ya kweli kama Isaya anavyoeleza katika Somo la Leo.
Isaya anawarudisha wana wa Israel kwenye asili yao, akiwahimiza kupanda, kujenga, kukua, na kuwasaidia wengine kufanya hivyo. Katika kusali na kufunga, waisraeli walikuwa wakifunga na kumlilia Mungu, wakitaka Mungu ajibu kulingana na kazi zao nzuri.
Mwanzoni, sura ya 58, inaakisi wana wa Israel kukata tamaa, kwa kutopata wanachostahili toka kwa Mungu. Isaya anawaambia labda ibada yao sio njema.
Vivyo hivyo;
Yesu anatupa maagizo tunavyopashwa kuenenda katika utukufu wa Mungu. Anatuita kuwa na ibada njema inayotafsiri maisha yetu. Yesu aliwaita wanafunzi, na Leo anatuita sisi kufanya zaidi ya tulivyozoea. Ibada sio "Mimi na Yesu" tu, bali ni pale tutambuapo, na tunapokuwa na uhusiano na Mungu wetu, kwa Yesu Kristo, anayetuunganisha na Mungu, na watu wote.
Ibada itufanye wenye njaa ya utukufu ujao, hivyo kuishi kama wafuasi wa Yesu Kristo hapa duniani. Njaa hii inawakilishwa kila tunapokusanyika kwa karamu takatifu, tunapoelezea uhusiano wetu wa karibu na Kristo, kwa kuungana pamoja karamuni, anayoiandaa Yesu. Tunakula "mkate wa uzima" na "kikombe cha wokovu" kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu.
Tuzingatie;
1. Ibada njema.
Ni kuishi maisha ya uchaji, yenye matendo ya huruma.
Tunapohudumia wahitaji, tunamtangaza kristo aliye uzima wetu.
2. Tunasisitizwa kutubu dhambi zetu.
Yesu alipoanza kazi yake hapa duniani, alianza hivi;
Mathayo 4:17
[17]Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.Ujumbe mkuu wa Kwaresma ni kuishi maisha ya toba na msamaha wakati wote.
Tunahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu kushinda dhambi.
Tunapokumbuka mateso ya Yesu, tuombe Neema ya Mungu, ili tuweze kuishi maisha ya ushindi, na hatimaye mbinguni.
Tubu na kurejea kwa Bwana.
Hii ni Kwaresma.