Date: 
24-03-2022
Reading: 
Isaya 28:24-29

Hii ni Kwaresma 

Alhamisi asubuhi tarehe 24.03.2022

Isaya 28:24-29

24 Je! Mwenye kulima alima daima, ili apande? Afunua daima madongoa ya nchi yake, na kuyavunja?

25 Akiisha kuulainisha uso wa nchi yake, je! Hamwagi huko na huko kunde, na kutupa-tupa jira, na kuitia ngano safu safu, na shayiri mahali pake palipochaguliwa, na kusemethi karibu na mipaka yake?

26 Kwa maana Mungu wake anamwagiza vizuri na kumfundisha.

27 Kwa maana kunde zile hazipurwi kwa chombo kikali, wala gurudumu la gari halipitishwi huko na huko juu ya jira ile, bali kunde zile hupurwa kwa fimbo, na jira ile kwa ufito.

28 Ngano ya mkate husagwa; kwa maana haipuri siku zote bila kukoma; na ingawa gurudumu la gari lake na farasi wake huitawanya ngano ile, haisagi.

29 Hayo nayo yatoka kwa Bwana wa majeshi, mwenye shauri la ajabu, apitaye wote kwa hekima yake.

Tutunze uumbaji;

Nabii Isaya anaonesha kuwa mtu anapoilima ardhi hutumia njia sahihi ili apate mavuno ya kutosha na mazuri. Hili ni agizo la Mungu kama somo linavyoonesha;

Isaya 28:26
26 Kwa maana Mungu wake anamwagiza vizuri na kumfundisha.

Isaya anatukumbusha nasi leo kutumia uumbaji wa Mungu kwa njia sahihi. Tutumie ardhi kwa ushauri wa kitaalamu ili ardhi itupe mazao bora. Tusiharibu wala kuchafua mazingira, maana kwa kufanya hivyo tunaumiza viumbe vingine. Haya ni maagizo ya Bwana kama tulivyosoma;

Isaya 28:29
Hayo nayo yatoka kwa Bwana wa majeshi, mwenye shauri la ajabu, apitaye wote kwa hekima yake.

Unayatimiza maagizo ya Bwana kwa kuutumia uumbaji wa Mungu kwa njia sahihi, zaidi kwa utukufu wake? Wajua kuwa kuchafua mazingira ni dhambi? Msikilize Bwana, kwa kutunza uumbaji wake.

Siku njema.