Date: 
12-07-2022
Reading: 
Isaya 1:1-9

Jumanne asubuhi tarehe 12.07.2022

Isaya 1:1-9

[1]Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi, aliyoyaona katika habari za Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.

[2]Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana BWANA amenena; 

Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi.

[3]Ng’ombe amjua bwana wake, 

Na punda ajua kibanda cha bwana wake; 

Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri.

[4]Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma.

[5]Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia.

[6]Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta.

[7]Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni.

[8]Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa.

[9]Kama BWANA wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.

Mungu ni mwingi wa huruma na haki;

Nabii Isaya anaandika juu ya Taifa ambalo halimchi Mungu. Anaonesha kwamba ng'ombe amjua bwana wake, punda ajua kibanda chake, lakini Israeli hawamjui Mungu wao! (3). Isaya anatoa ole kwa Taifa lisilomcha Mungu. Anakazia kuwa kwa neema ya Mungu, Israeli hawakuwa kama Sodoma na Gomora.

Ujumbe huu unatuita kujihoji na kutambua kama tunamcha Bwana. Tunaalikwa kujichunguza kama njia zetu zinafaa, zinampendeza Mungu. Sisi ni wenye haki mbele za Mungu mwenye huruma? 

Tunaishi kwa sababu ya neema yake, hivyo tunawajibika kumcha, tukimtumikia kwa uaminifu sasa na siku zote. Amina.

Siku njema