Event Date: 
03-06-2021

Siku ya Jumapili, 30/5/2021, lilifanyika tamasha la uimbaji ambalo lilishirikisha kwaya sita zinazohudumu katika Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral chini ya usimamizi wa Kamati ya Uinjilisti ya usharika ikiongozwa na mwenyekiti wake Mzee Simon Jengo.

Mbali ya uimbaji, tamasha hilo liliambatana na semina iliyofunguliwa na Mchungaji Joseph Mlaki aliyefundisha juu ya asili ya uimbaji akitumia somo kutoka katika kitabu cha Zaburi 146:1-2. Mchungaji Mlaki aliwaasa waimbaji kuimba kwa furaha na kwa kumsifu Bwana.

Katika hatua nyingine, Mchungaji Gwakisa Mwaipopo ambaye pia alishiriki kikamilifu katika tamasha hilo, alitoa fundisho fupi kwa kuwasisitizia washiriki kuwa uimbaji ni mali ya Bwana, kwani kila kilichoumbwa na Bwana ni chake. Aliyasema hayo akitumia neno takatifu kutoka katika kitabu cha Wakolosai 1:15-17. Pia aliwaeleza waimbaji kuwa ni vyema kukaa pamoja kwa kupendana wakiwa katika huduma ya uimbaji, alitumia kitabu cha Zaburi 133:1.

Mchungaji Mwaipopo alionya juu ya migogoro katika vikundi mbalimbali vya usharika. “Kila mtu akae katika nafasi yake aliyobarikiwa na Mungu.  Hapa hatuimbi kwa ajili ya kuwafurahisha au kuwakomoa watu fulani bali tunaimba kwa ajili ya kumwabudu Mungu wetu. Mungu alipotupa hivi vipawa ilikuwa ni kwa ajili ya kusaidiana na sio kujikweza mbele za wengine na kusababisha migogoro katika vikundi vyetu.”

Pia mtumishi Peter Maoga alifundisha somo la faida za uimbaji akitumia somo kutoka katika kitabu cha 1 Mambo ya Nyakati 20:5-22. Aliwasisitiza waimbaji kwa kusema, “Bwana husifiwa kwa uimbaji na hushusha utukufu kwa njia ya uimbaji”. Pia alisema kupitia uimbaji inapatikana tiba na badiliko la moyo.

Katika tamasha hilo lililojaa mahubiri kupitia njia ya uimbaji lilishirikisha Kwaya Kuu, Kwaya ya Upendo, Kwaya ya Wanawake, Kwaya ya Agape, Kwaya ya Vijana pamoja na Kwaya ya Tarumbeta. Pia vijana wawili wadogo, Brian Foy na Rajev walioonyesha ufundi wao wa kupiga piano.

Mwenyekiti wa vikundi vya usharika Bi. Dorothy Buchanagandi, aliwashikuru waimbaji kwa kuitikia wito wa kuimba katika tamasha hilo na akawasihi wawe wanajumuika pamoja na kuitika wito wa kuimba pindi wanapoombwa kuimba pamoja kwa ajili ya kumtumikia Mungu.

Tamasha hilo lilifungwa na Mchungaji Kiongozi wa Usharika, Mch Charles Mzinga ambaye aliwashukuru waimbaji wote kwa kufanikisha tamasha hilo huku akiwasihi kuendelea kujumuika katika uimbaji na kumtumikia Mungu kwa moyo na kwa kujitoa bila kuweka masharti na majivuno mbele. “Tuendelee na moyo wa kumtumikia Mungu kwa uaminifu na kila mmoja asimame katika nafasi yake”, alisema.

Baadhi ya matukio katika Picha.

 

Walioshiriki kuandaa ripoti hii ni: Jane Mhina/Paulin Paul