Siku ya Jumapili, tarehe 30/10/2022, Usharika wa KKKT Kanisa Kuu Azaniafront Cathedral ulifanya maadhimisho ya sikukuu ya mavuno pamoja na sikukuu ya matengenezo ya kanisa. Sikukuu ya mavuno hufanyika kila mwaka ili kutoa fursa kwa washarika kumtolea Mungu sehemu ya matunda au mavuno ya kazi wanazozifanya.
Ibada ya kusherehekea sikukuu hii ya mavuno kwa mwaka 2022 imefanyika katika viwanja vya usharika wa Kanisa Kuu Azania Front huku ikihudhuiriwa na mamia ya washarika waliojitokeza kwa wingi wakiwa na mavuno yao tayari kwa kumtolea Mungu.
Ibada hiyo imeongozwa na Msaidizi wa Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza akisaidiana na Mchungaji Kiongozi wa Usharika Chaplain Charles Mzinga, Mchungaji Joseph Mlaki na Mchungaji Gwakisa Mwipopo.
Msaidizi wa Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza (katikati), Mchungaji Kiongozi wa Usharika Chaplain Charles Mzinga (kushoto) pamoja na Mchungaji Joseph Mlaki (kulia) wakati wa ibada ya Mavuno 2022.
Dean Chediel Lwiza akishiriki ibada ya Mavuno kwenye Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral.
Akizungumza wakati wa Ibada hiyo, Dean Chediel Lwiza aliwakumbusha washarika wa Azania Front kujenga tabia ya kujitokeza kwa wingi kuhudhuria ibada hiyo huku akisisitiza umuhimu wa sikukuu ya hiyo katika maisha ya kikristo.
“Sadaka ya Mavuno ni tofauti kabisa na sadaka nyingine zote kwa sababu inatolewa mara moja kwa mwaka. Ukiona kila ulicho nacho, unapumua, unaongea, unatembea, una afya; mshukuru Mungu. Sadaka hii inabidi itoke kwenye kilindi cha moyo wako,” alisema.
“Lazima umkumbuke Mungu kwa sababu amekulinda wakati wote yeye mwenyewe. Kumbuka yeye ndiye anayekupa nguvu za kutembea na kukuwezesha kuvuka milima na mabonde na kila aina ya changamoto unayokutana nayo,” aliongeza.
Ibada ya sikukuu ya mavuno katika Usharika wa Azania Front imehudhuriwa na washarika na vikundi vyote vya usharika ambapo ibada ilitanguliwa na maandamano mafupi na utoaji wa sadaka pamoja na mavuno yenyewe huku ikihitimishwa kwa mahubiri kutoka kwa Dean Chediel Lwiza na mwsiho kabisa ukifanyika mnada wa bidhaa au mavuno yaliyokuwa yamewasilishwa na washarika.
Kwaya ya Usharika ikiimba wakati ibada ya Mavuno.
Pia Kwaya ya Vijana kutoka Usharika wa Mabibo Farasi iliungana na Kwaya za Usharika wa Azania Front Cathedral katika kuipamba ibada hiyo kupitia tungo mbalimbali za kumtukuza Bwana wetu.
------------------------------
Neno Lililotumika: Kumbukumbu la Torati 8: 11 - 18
11Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. 12 Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; 13 Na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; 14 Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; 15 Aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, 16 Aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. 17 Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. 18 Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.
Washarika wa Azania Front wakitoa sadaka ya Mavuno
Washarika wa Azania Front wakitoa sadaka ya Mavuno
Washarika wa Azania Front wakitoa sadaka ya Mavuno
------------------------------------------------------------------
Angalia Picha: Ibada ya Mavuno 2022
Tazama AZFTV: Ibada ya Mavuno 2022