Alhamisi asubuhi tarehe 21.07.2022
Ayubu 42:1-8
[1]Ndipo Ayubu akamjibu BWANA, na kusema.
[2]Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote,
Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.
[3]Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa?
Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu,
Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua.
[4]Sikiliza, nakusihi, nami nitanena;
Nitakuuliza neno, nawe niambie.
[5]Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio;
Bali sasa jicho langu linakuona.
[6]Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu
Katika mavumbi na majivu.
[7]Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
[8]Basi sasa, jitwalieni ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
Tunaitwa kuwa wanafunzi na wafuasi;
Ayubu alipitia shida nyingi. Alipoteza watoto, mifugo na mali nyingine zote. Wengi walikuwa kinyume naye akiwemo mke wake, wakimwekea mazingira ya kumuacha Bwana baada ya kuumwa sana. Sasa leo asubuhi tunaona wale marafiki wa Ayubu wakielekezwa kwenda kwa Ayubu na sadaka akawaombee ili Mungu asiwaadhibu kwa upumbavu wao maana hawakunena maneno yaliyonyooka, kama alivyonena Ayubu.
Ushuhuda wetu kwa wengine kuhusu Kristo ukoje? Tunanena maneno yaliyonyooka kuhusu ufalme wa Mungu? Maneno yetu yanawafanya wengine kuwa wanafunzi na wafuasi wa Yesu?
Tukishuhudia isivyostahili tunamchukiza Mungu, maana hatuwezi kuwa mashuhuda wema wa Injili kwa wengine. Ishuhudie kweli usiadhibiwe na Bwana. Unashuhudiaje? Waza, nena na kutenda yakupasayo kama mfuasi na mwanafunzi wa Yesu.
Siku njema.