Hii ni Kwaresma
Jumamosi asubuhi tarehe 18.03.2023
Ayubu 38:27-41
27 Kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, Na kuyameza majani yaliyo mororo?
28 Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?
29 Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?
30 Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi.
31 Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni?
32 Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake?
33 Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia?
34 Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize?
35 Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa?
36 Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni?
37 Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni?
38 Wakati mavumbi yagandamanapo, Na madongoa kushikamana pamoja?
39 Je! Utamwindia simba mke mawindo? Au utashibisha njaa ya simba wachanga,
40 Waoteapo mapangoni mwao, Wakaapo mafichoni wapate kuvizia?
41 Ni nani anayempatia kunguru chakula, Makinda yake wanapomlilia Mungu, Na kutanga-tanga kwa kutindikiwa na chakula?
Tutunze mazingira;
Leo asubuhi tunasoma juu ya hali ya hewa kama matokeo ya uumbaji wa Mungu. Ayubu anaandika jinsi mvua inyeshavyo kuleta mvua na kuwezesha mimea kukua, pia maji ya kunywa kwa wanyama na binadamu. Katika mstari wa mwisho (41) tunaona jinsi ambavyo uumbaji wa Mungu huwezesha viumbe hai kupata chakula. Yote hii ni matukio ya uumbaji.
Katika uumbaji, mahitaji yote hupatikana kwa viumbe vyote katika uumbaji huo huo. Tumeona ambavyo maji ni muhimu kwa wanyama na mimea. Yote hiyo ni matokeo ya uumbaji. Kumbe tunapashwa kutunza uumbaji wa Mungu ili ututunze.
Jumamosi njema.
Heri Buberwa