Jumanne asubuhi tarehe 01.02.2022
2 Wafalme 5:1-8
1 Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma.
2 Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani.
3 Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.
4 Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi.
5 Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi.
6 Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake.
7 Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami.
8 Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.
Tunalindwa na nguvu za Mungu;
Tumesoma habari za Naamani Jemedari wa jeshi la Shamu, ambaye pamoja na ujemedari wake alikuwa na ugonjwa wa ukoma. Tunasoma akiletewa ujumbe kuwa akienda kwa mfalme wa Israeli yupo nabii anaweza kumsaidia kupona.
Tunaitwa kuwa wasikilizaji na watendaji wa neno la Mungu. Naamani aliletewa neno akalifanyia kazi (tutaona katika somo la jioni). Wewe unalisikia neno la Mungu na kulifanyia kazi? Unajua kuwa bila kulifanyia kazi neno la Mungu unajidanganya nafsi yako?
Yakobo 1:22 Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.Msikilize Mungu anaposema na wewe, ndipo utafanikiwa. Hauwezi kufika popote bila msaada wake, maana sisi tunalindwa na nguvu za Mungu.
Siku njema.