Date: 
15-08-2022
Reading: 
2 Petro 2:18-22

Jumatatu asubuhi tarehe 15.08.2022

2 Petro 2:18-22

[18]Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu;

[19]wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.

[20]Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.

[21]Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.

[22]Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.

Hekima ituingizayo mbinguni;

Petro anaandika juu ya manabii wa uongo wanenao maneno ya kiburi kwa tamaa zao, wakiwadanganya watu wa Mungu. Huwaahidi watu kufunguliwa, kumbe sio manabii wa kweli, bali watumwa wa uharibifu. Huwa wako tayari kufanya lolote wafanikiwe kupitia kwa watu, lakini siyo kusaidia kundi la Mungu. Wanajisaidia wao, ni wabinafsi, waongo, wezi, wasio na huruma. Neno la Mungu ni kwa ajili ya kuokoa watu na siyo kuwapoteza. 

Petro anawaonya kuwa adhabu ya Mungu iko juu yao kwa sababu ya kuwapoteza watu wa Mungu. Sisi wajibu wetu ni kuomba neema ya Mungu ili tutambue unabii wa uongo na kuuepuka. Yesu afanyike hekima kwetu ili tuwaepule manabii wa uongo. 

Uwe na wiki njema yenye ushuhuda.