Date: 
18-04-2022
Reading: 
1Korintho 6:14

Jumatatu ya Pasaka;

Jumatatu ya tarehe 18.04.2022

Kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo;

Masomo;

Zab 134:1-3

Mk 16:12-13

*1Kor 6:14

1 Wakorintho 6:14 Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza wake.

Tembea na Yesu mfufuka;

Katika Sura ya sita ya waraka wa kwanza kwa Wakorintho, Mtume Paulo anaendelea kukabiliana na waamini wa Korintho juu ya mambo mbalimbali katika Kanisa. Sura tangulizi zinajadili migawanyiko katika Kanisa na mienendo mibaya katika suala la ndoa. Paulo anawaonya kuwa waangalie wasije kupelekana mbele ya mahakama kwa mambo madogo. Badala ya kushtakiana mbele ya hata wasioamini, wasikilizane na kuelewana Kanisani. Pia Paulo anawasihi waishi kwa imani yao kama walivyompokea Kristo, badala ya kutofuata sheria na taratibu za ndoa. Hii inapeleka mjadala wa ndoa katika sura ya saba.

Somo lenyewe;

Mtume Paulo katika mstari wa 12 hadi 20 anakataa mawazo na njia mbaya za maisha zisizofaa kuhusu ndoa na maisha kwa ujumla, kwa watu wa Kanisa la Korintho. Paulo anahimiza kufuata taratibu za kimaadili katika maisha ya waaminio. Paulo anaonesha kuwa Mungu aliamua wawili waungane na kuwa mwili mmoja, wakiacha uzinzi na ukahaba, na si vinginevyo. Paulo anajenga hoja juu ya uchaji katika maisha ya waunganao, ili wajitunze miili yao kwa maana miili ya waaminio ni hekalu la Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hakai hekalu chafu!

Wakati ule watu hawakujali jinsi walivyoishi, na nafasi ya miili yao katika zinaa!! Paulo anawaeleza;

1 Wakorintho 6:12-13

12 Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote.
13 Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili.

Watu walitumia vibaya neema, kwamba wangefanya lolote na Mungu angekuwa nao. Paulo analikataa jambo hili! Ndipo Mtume Paulo anakuja leo na ujumbe huu;

1 Wakorintho 6:14 Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza wake.

Paulo alimaanisha nini kwa Wakorintho?

1. Mungu aliyemfufua Kristo Yesu, ni mwenye nguvu, utukufu na uwezo.

Mtume Paulo anawasihi Wakorintho kuacha kuishi maisha ya mazoea, na badala yake wamche Mungu mwenye nguvu, uwezo na utukufu. 

Utukufu wa Mungu hauna ubia, ndio maana Paulo aliwausia kuacha uovu.

2. Yesu mfufuka, anatusamehe na kutupokea.

Paulo anaposema "...atatufufua sisi kwa uweza wake..." anamaanisha kuwa Yesu ndiye mwokozi, aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu. Yu tayari kutufufua, yaani kututoa dhambini. 

Sauti ya Yesu inatuita leo kutoka dhambini, tuishi maisha ya toba na msamaha tukiwa wenye imani ya kweli.

Matumizi mabaya ya neema aliyakataa Mtume Paulo.

Kuishi tunavyotaka tukisema neema ya Mungu ipo siyo sahihi. Neema ya Mungu ipo kwa kila aaminiye ikiambatana na wajibu ambao ni kutubu, kuamini na kumgeukia Yesu, yaani kutembea na Yesu mfufuka.

Ibada njema.