Date: 
25-04-2022
Reading: 
1 Samweli 9:15-21

Jumatatu asubuhi tarehe 25.04.2022

1 Samweli 9:15-21

15 Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema,

16 Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia.

17 Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.

18 Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi?

19 Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako.

20 Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?

21 Basi Sauli akajibu, akasema, Je! Mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? Na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila ya Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo?

Yesu Kristo ajifunua kwetu;

Mungu alimtuma Samweli kumpaka mafuta Sauli, yaani kumweka wakfu kuwa kiongozi wa watu wake. Sauli alienda nyumbani kwa Samweli akalala usiku mmoja, na asubuhi yake Samweli akamweka wakfu. 

Wakati wa Agano la kale Mungu alijifunua kwa watu wake yeye mwenyewe, na (au) kupitia kwa watu kama tulivyoona. Leo Yesu anajifunua kwetu mwenyewe, akituita kumuamini na kumfuata katika safari yetu ya imani, kwa maisha ya sasa na baadaye. Uwe na wiki njema.