Date: 
20-08-2022
Reading: 
1 Samweli 15:10-23

Jumamosi asubuhi tarehe20.08.2021

1 Samweli 15:10-23

[10]Ndipo neno la BWANA likamjia Samweli, kusema,

[11]Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia BWANA usiku kucha.

[12]Samweli akaondoka asubuhi na mapema ili aonane na Sauli; Samweli akaambiwa ya kwamba, Sauli alifika Karmeli, na tazama, akajisimamishia ukumbusho, akageuka, akapita, akatelemkia Gilgali.

[13]Samweli akamwendea Sauli; naye Sauli akamwambia, Ubarikiwe na BWANA, nimeitimiza amri ya BWANA.

[14]Samweli akasema, Maana yake nini, basi, hiki kilio cha kondoo masikioni mwangu, na huu mlio wa ng’ombe ninaousikia?

[15]Sauli akasema, Wamewaleta kutoka kwa Waamaleki; maana watu waliwaacha hai kondoo na ng’ombe walio wazuri, ili wawatoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, nao waliosalia tumewaangamiza kabisa.

[16]Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia BWANA usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema.

[17]Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye BWANA akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli.

[18]Kisha BWANA akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia.

[19]Mbona, basi, hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA?

[20]Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya BWANA, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.

[21]Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali.

[22]Naye Samweli akasema, 

je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu 

Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? 

Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, 

Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.

[23]Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, 

Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; 

Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, 

Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.

Hekima ituingizayo mbinguni;

Msingi wa somo hili ni lile somo la jana usiku (lisome tena) ambapo Sauli alitumwa kuangamiza WaAmaleki hakuwaangamiza wote na mifugo pia. Neno la Bwana linamjia Samweli aliyemtawaza Sauli kuwa mfalme kuwa Sauli hakuitii sauti ya Mungu. Sauli alijaribu kujitetea lakini Samweli akamwambia kuwa kwa kutokutii sauti ya Mungu, Sauli alikataliwa na Mungu kuwa Mfalme.

Sisi tunaongozwa na neno la Mungu. Mungu anapenda na anataka tumtii. Yaani anapenda utii kuliko sadaka (mst 22).

Kutokutii ni hatari sana katika maisha ya kila aaminiye. Biblia ni neno la Mungu na halina mbadala, hivyo Biblia kama neno la Mungu ndiyo msingi wa Kanisa. Kutoutii msingi wa Kanisa ni kupotea. Hekima ya kiMungu hutuongoza kumtii Kristo na hatimaye kuurithi uzima wa milele.

Uwe na Jumamosi njema.