Date: 
29-08-2022
Reading: 
1 Petro 5:5-7

Jumatatu asubuhi tarehe 29.08.2022

1 Petro 5:5-7

[5]Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.

[6]Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;

[7]huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.

Iweni wanyenyekevu;

Sura ya tano ya waraka wa kwanza wa Petro ni fundisho juu ya kuchunga kundi la Mungu. Petro analiambia Kanisa kufanya kazi hiyo kwa hiari, na si kwa kulazimishwa. Katika utume, ndipo anaiasa jamii ya waaminio kukaa pamoja, vijana wakiwatii wazee na watu wote wakihudumiana kwa upendo. Tunaona kuwa kukaa pamoja kunahusisha unyenyekevu, kama Petro anavyoandika.

Kazi tuliyoitiwa tunaifanya kila siku, lakini je, tunaifanya tulivyoagizwa? Tunapendana? Tunaheshimiana? 

Haya yote na mengine kama hayo hayawezi kutokea kama mmoja akijiona bora kuliko mwenzake. Tunaalikwa kuhudumiana kwa upendo, tukitenda kazi ya Mungu kwa pamoja. Katika kazi hiyo, tuwe wanyenyekevu ili Mungu atukweze kwa wakati wake, maana yeye huwapinga wenye kiburi na kuwapa wanyenyekevu neema.

Uwe na wiki njema.