Date:
09-09-2022
Reading:
Zaburi 45:1
Ijumaa asubuhi tarehe 09.09.2022
Zaburi 45:1
[1]Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi.Tutumie vizuri ndimi zetu;
Moyo uliojaa neno jema humpa mtu kusema yaliyo mema. Ni kwa sababu mhusika huwa vizuri, kwa sababu moyo wake umejaa mambo mema. Hivyo huwa vyema, kwa sababu yasemwayo huwa mema, na Mungu husifiwa. Ndiyo maana katika kusema mema huku, mwimbaji wa Zaburi anafananisha ulimi wake na kalamu mstadi.
Tunaalikwa kutafakari na kujihoji kama mioyo yetu ni safi, kiasi cha sisi kutamka yaliyo mema. Mioyo yetu ikijawa mambo mema basi tutasema vema. Hata Yesu alisema;
Luka 6:45
[45]Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.Neema ya Mungu iwe juu yetu, ili mioyo yetu ijae mambo mema, ndipo tutaweza kutumia ndimi zetu kwa Utukufu wa Mungu.
Siku njema