Hii ni Pasaka;
Jumanne asubuhi 05.05.2026
Kutoka 15:16-21
[16]Hofu na woga umewaangukia;
Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe;
Hata watakapovuka watu wako, Ee BWANA,
Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.
[17]Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako,
Mahali pale ulipojifanyia, Ee BWANA, ili upakae,
Pale patakatifu ulipopaweka imara, BWANA, kwa mikono yako.
[18]BWANA atatawala milele na milele.
[19]Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, BWANA akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari.
[20]Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.
[21]Miriamu akawaitikia,
Mwimbieni BWANA kwa maana ametukuka sana;
Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.
Njooni tumsifu Mungu wetu;
Somo tulilosoma ni maneno ya wimbo wa Israel baada ya kuvuka bahari ya Shamu. Wanamshukuru na kumsifu Bwana aliyewaokoa na jeshi la Farao. Walimuona Bwana aliyetukuka, wakamwimbia sifa wakimshukuru kwa kulitupa baharini jeshi la Farao na kuliangamiza.
Mungu alionyesha kuwa yuko nao. Aliwaokoa. Alikuwa amejifunua kwao kwa kiwango kikubwa sana. Ndivyo Bwana Yesu anavyojifunua kwetu hata sisi leo, akidhihirisha kuwa yuko nasi, anatupenda, anatujali, lakini zaidi ni Mwokozi.
Kwa kufa na kufufuka, Yesu amejifunua kwetu kama Mwokozi wetu, hivyo anastahili sifa. Tumsifu daima, tukimpa mioyo yetu aitawale na kutupa mwisho mwema. Amina
Uwe na siku njema mwema
Heri Buberwa
