Date: 
04-05-2026
Reading: 
Marko 14:26

Hii ni Pasaka;

Jumatatu asubuhi tarehe 04.05.2026

Marko 14:26

Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.

Njooni tumsifu Mungu wetu;

Ulikuwa ni utaratibu wa kawaida kuimba ibadani, utaratibu ambao Kanisa la leo limeurithi. Kwa somo la leo asubuhi, ni siku ya kuanzishwa kwa ushirika Mtakatifu, ambapo Yesu anaanzisha chakula cha Bwana kabla ya kusulibiwa. Ibada hiyo iliambatana na uimbaji, na baada ya kuimba ndipo wakaondoka kuelekea mlima wa Mizeituni. Inaaminika kwa siku hizi walikuwa wakiimba Zaburi 113 hadi 118, ambazo huitwa "Hallel Psalms", ikiwa ni sehemu ya sherehe za Pasaka. Sehemu ya Zaburi tajwa hapo juu ndiyo imechukuliwa kuimba wakati wa Pasaka kama tuimbavyo;

Zaburi 118:15-17, 22-24

15 Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.

16 Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.

17 Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.

22 Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

23 Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu.

24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

Somo linaonesha utaratibu wa uimbaji tangu kale kama tufanyavyo leo, uimbaji unaomsifu Mungu. Tukumbushane kumsifu Mungu wetu kwa mashangilio. Nyimbo zetu zinakuwa za sifa kwa Mungu tunapoimba katika kweli tukitenda yatupasayo. Maisha yetu yakiwa yenye ushuhuda, wimbo wetu unakuwa mpya siku zote. Amina

Tunakutakia wiki njema yenye kumsifu Mungu 

 

Heri Buberwa Nteboya

Mlutheri 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com