Date: 
01-05-2026
Reading: 
Zaburi 86:11-17

Hii ni Pasaka;

Ijumaa asubuhi tarehe 01.05.2026

Zaburi 86:11-17

11 Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako; Moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako;

12 Nitakusifu Wewe, Bwana, Mungu wangu, Kwa moyo wangu wote, Nitalitukuza jina lako milele.

13 Maana fadhili zako kwangu ni nyingi sana; Umeiopoa nafsi yangu na kuzimu.

14 Ee Mungu, wenye kiburi wamenishambulia; Mkutano wa wakatili wamenitafuta roho. Wala hawakukuweka Wewe Mbele ya macho yao.

15 Lakini Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema, Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli.

16 Unielekee na kunifadhili mimi; Mpe mtumishi wako nguvu zako, Umwokoe mwana wa mjakazi wako.

17 Unifanyie ishara ya wema, Wanichukiao waione na kuaibishwa. Kwa kuwa Wewe, Bwana, Umenisaidia na kunifariji.

Ndani ya Kristo tunakuwa wapya;

Tunauanza mwezi wa tano kwa kumsoma Daudi akiimba wimbo ambao ni sala ya kuomba msaada toka kwa Mungu. Anaomba Mungu amfundishe njia yake, akiahidi kumsifu kwa moyo na kulitukuza jina lake milele. Daudi anakiri fadhili za Bwana kuwa nyingi, anakiri ushindi kwa msaada wa Bwana. Anaendelea kuomba ishara ya wema kwa wote wanaomzunguka.

Kama Daudi alivyoimba akiomba msaada wa Bwana, nasi tunakumbushwa kwamba hatuwezi kuenenda peke yetu bila msaada wa Bwana. Tunahitaji msaada wa Yesu Kristo mfufuka ili tuweze kutenda yaliyo mapenzi yake. Inawezekana kwa msaada wake. Amina

Ijumaa njema

 

Heri Buberwa