Date: 
14-03-2025
Reading: 
Danieli 3:24-30

Hii ni Kwaresma 

Ijumaa asubuhi tarehe 14.03.2025

Danieli 3:24-30

24 Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme.

25 Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.

26 Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto.

27 Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo.

28 Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.

29 Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.

30 Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli.

Mungu hutuwezesha kushinda majaribu;

Mfalme Nebukadreza alitengeneza sanamu ya dhahabu, na siku ya kuizindua walialikwa watu wote, kuanzia wale mashuhuri na wengine wote. Watu wote walitakiwa kuiinamia na kuiabudu sanamu. Yeyote ambaye hakuiabudu sanamu alitangaziwa kutupwa kwenye tanuru la moto. 

Shadrack, Meshack na Abednego walikataa kuiabudu sanamu ya Mfalme. Angalia walivyojibu;

Danieli 3:16-18

16 Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili.
17 Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.
18 Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.

Ndipo katika somo la leo asubuhi tunasoma Mfalme Nebukadreza akikasirika na kuamuru watupwe kwenye tanuru la moto. Hawakuungua! Walitoka wazima kama walivyoingia! Mfalme akatangaza kuwakuza Shadraka, Meshaki na Abednego katika Babeli. Shadraka, Meshaki na Abednego walikataa kuabudu sanamu, wakapona kuungua kwenye tanuru la moto. Nasi tukimtegemea Mungu tutashinda majaribu. Amina.

Ijumaa njema

Heri Buberwa