Date: 
03-07-2024
Reading: 
Yohana 13:12-15

Jumatano asubuhi tarehe 03.07.2024

Yohana 13:12-15

12 Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea?

13 Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo.

14 Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.

15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

Ninyi ni barua ya Kristo;

Kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alikuwa ameketi chakulani na wanafunzi wake. Ili hali akijua saa yake imewadia alikwenda pembeni akajifunga kitambaa kiunoni akaanza kuwatawadha wanafunzi wake miguu. Ndipo tumesoma akiwauliza wanafunzi wake kama walielewa maana ya tukio lile, akiwaelekeza watende kama alivyowatendea. 

Yesu alionesha upendo wake kwa kuwatawadha wanafunzi wake miguu. Aliwatawadha wote, akiwemo hata yule ambaye angemsaliti (Yuda Iskariote). Tabia ya Yesu ni upendo na huruma kwa watu wote. Nasi anatualika kuwa kama yeye, yaani tupendane na kutendeana wema siku zote maana sisi ni barua ya Kristo. Amina.

Jumatano njema.

Heri Buberwa