Date: 
12-06-2024
Reading: 
Wakolosai 3:12-17

Jumatano asubuhi tarehe 12.06.2024

Wakolosai 3:12-17

12 Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,

13 mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

14 Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.

15 Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.

16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.

17 Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.

Heri wenye moyo safi;

Mtume Paulo anawaambia Wakolosai kuwa wao ni wateule, kwa maana ya kwamba wanamwamini Kristo. Anawaita kuwa na moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, utii, msamaha, upendo, na mengine kama hayo, amani ya Mungu ikiwa ndani yao. Muhimu kuliko yote anawasihi kuwa na neno la Kristo ndani yao ili waweze kuushinda Ulimwengu. 

Mtume Paulo anasisitiza kufanya yote katika jina la Yesu Kristo kama tulivyosoma mstari wa 17;

Wakolosai 3:17

Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.

Asubuhi hii tukumbuke kulishika neno la Mungu, ambalo ni mwongozo usiokosea. Kwa njia ya neno la Kristo tunayo nafasi ya kutenda mambo yote kwa Utukufu wa Mungu. Tunakuwa na moyo safi kwa kulishika neno la Kristo. Amina.

Jumatano njema 

 

Heri Buberwa 

Mlutheri