Date: 
07-06-2024
Reading: 
1 Wafalme 8:22-24

Ijumaa asubuhi tarehe 07.06.2024

1 Wafalme 18:22-24

22 Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini.

23 Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini.

24 Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.

Chagueni mtakayemtumikia;

Jana asubuhi tuliona Eliya akimwambia Ahabu kuwa nchi ilikuwa na njaa kwa sababu watu waliziacha amri za Bwana. Akamwambia kuwaita jamii ya Israeli, manabii wa Ashera, Baali na wengineo. Akaamuru walete mnyama kwa ajili ya sadaka, Halafu akawaambia wamuite Mungu ashushe moto kuipokea sadaka. Hakuna mungu aliyeitika, yaani huyo mungu wa Baali hakuitika.

Sasa ukiendelea kusoma unaona Eliya akitengeneza madhabahu, anaweka sadaka na kuamuru imwagiwe mapipa ya maji mara tatu. Halafu anamuita Mungu anashusha moto, na kuipokea sadaka. 

Soma hapa;

1 Wafalme 18:37-39

37 Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.
38 Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.
39 Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.

Tukio la Mungu kuitikia sala ya Eliya liliwafanya watu waanguke kifudifudi na kukiri kuwa Bwana ndiye Mungu. Walichagua kumtumikia Bwana. Wokovu tuliopewa kwa neema na baraka tunazopewa kila siku ni sababu tosha kabisa ya kuchagua kumtumikia Bwana. 

Chagua kumtumikia Yesu Kristo daima. Amina.

Ijumaa njema.

Heri Buberwa