Date: 
03-04-2024
Reading: 
1Petro 1:8-13

Jumatano asubuhi tarehe 03.04.2024

1 Petro 1:18-23

18 Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;

19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.

20 Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu;

21 ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

22 Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo.

23 Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.

Tunaitwa kutembea na Yesu mfufuka;

Petro anaanza waraka wake wa kwanza kwa udhihirisho wa wanadamu kukombolewa kwa damu ya Yesu Kristo. Anamtukuza Mungu ambaye aliuokoa ulimwengu, kwa ahadi ya kuurithi uzima wa milele. Katika kusisitiza hili Petro anasema;

1 Petro 1:3-4

3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;
4 tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.

Kwa kukazia wokovu kwa wanadamu, katika somo tulilosoma Petro anawakumbusha wasomaji wake kwamba hawakukombolewa kwa vitu vya dunia viharibikavyo, bali kwa damu ya thamani, kama ya Mwana Kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani ya Kristo. Petro alilazimika kutumia lugha ya Mwana Kondoo kwa sababu jamii ya wakati ule ilikuwa na historia ya kukombolewa kwa damu ya mwanakondoo aliyeteketezwa. Sasa Petro anawaandikia kuwa ukombozi ni kwa damu ya Yesu Kristo.

Anachokisema Petro ni kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana Kondoo wa Pasaka aliyejitoa kufa mara moja msalabani na kuwaokoa watu wote. Katika mstari wa 24, Petro anasema Kristo huyu aliyemwaga damu yake kutukomboa ndiye neno lenye uzima, lidumulo hata milele. Tutembee naye maishani mwetu siku zote, ili tuurithi uzima wa milele. Amina.

Jumatano njema 

Heri Buberwa