Date: 
01-04-2024
Reading: 
Yohana 20:24-29

Hii ni Pasaka 

Jumatatu ya Pasaka tarehe01.04.2024

Masomo;

Zab 89:15-21

1Pet 1:18-23

*Yn 20:24-29

Yohana 20:24-29

24 Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu.

25 Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.

26 Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu.

27 Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.

28 Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu!

29 Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.

Tunaitwa kutembea na Yesu mfufuka;

Injili ya Yohana inaelezea kwa mpangilio mzuri, matukio manne muhimu yanayoonyesha Yesu akijidhihirisha kwa watu kwamba yu hai tena.

1) Alimtokea Mariamu Magdalena kaburini aliyedhani mwili wa Yesu umeibwa;

Yohana 20:14-18

[14]Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu.
[15]Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.
[16]Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu wangu).
[17]Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.
[18]Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.
2) Alipofufuka aliwatokea wanafunzi kumi, kasoro Thomaso ambaye hakuwa pamoja na wenzake waliojifungia kwa hofu ya wayahudi.

Yohana 20:19-20

[19]Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu.
[20]Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.

3) Aliwatokea wanafunzi kumi na moja, akiwamo Thomaso, ili naye apate kusadiki kuwa Yesu kafufuka.

Yohana 20:26-27

[26]Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu.
[27]Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.

(Hapa ndipo kuna somo la leo)

4)Alijidhihirisha kwa wanafunzi wake akiwa katika bahari ya Tiberia, ikiwa ni mara ya tatu kujifunua kwa wanafunzi.

Yohana 21:1-2

[1]Baada ya hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi.
[2]Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja.

Sasa tukirudi kwenye somo la leo;

Tunamuona Yesu akijidhihirisha kwa mara ya tatu, ikiwa ni mara ya pili akiwatokea wanafunzi (rejea mtiririko hapo juu) Thomaso akiwepo, maana alipowatokea kabla, Thomaso hakuwepo. Thomaso anaonekana kuwa mhusika mkuu katika tukio hili. Hivyo ni muhimu tukamuangalia kidogo huyu Thomaso.

-Thomaso alikosa wasaa wa kumuona Yesu mapema, tofauti na wenzake, maana alijitenga. 

Hakuwa katika ushirika na wenzake.

Haielezwi alikuwa wapi katika sehemu hii.

Alikuwa mgonjwa? Alipata dharura? Alikuwa wapi?!

Lakini iwe vyovyote, picha tunayoiona ni wanafunzi kukaa katika ushirika, kwa pamoja.

Alipowatokea mara ya kwanza, aliwapa baraka;

Yohana 20:22-23

[22]Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.
[23]Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

Thomaso aliikosa baraka hii kwa wakati huu!

Hapa tunaona Yesu akitufundisha kukaa pamoja, sisi kama familia ya Mungu, tukidumu katika ushirika wa pamoja. Yaani Kanisa liwe na umoja. Tunapoishi na kuitenda kazi ya Mungu, tuongozwe kwa pamoja na Yesu Kristo, na tusikubali mmoja wetu abaki nyuma. Kila mmoja atamani kukaa katika ushirika na wakristo wenzake, maana sisi tu mwili mmoja kama tunavyokumbushwa kila tunaposhiriki Sakramenti ya madhabahu;

1 Wakorintho 10:16-17

[16]Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?
[17]Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

-Thomaso alikuwa mtu wa vitendo, mwenye kutaka ushahidi wa Kisayansi.

Alitaka kumuona Yesu hadharani, tena aguse sehemu zilizoumizwa ndipo aamini kuwa kweli Yesu kafufuka. Ni pale alipowaambia wenzake kuwa asipoiona kovu za misumari asingeamini. 

Thomaso anatanguliza uhalisia wa macho ili aamini.

Ni kweli Sayansi, na hatuwezi kuikwepa, maana Sayansi inaongoza maisha yetu kwa sehemu. Shida ni pale tunapoitanguliza Sayansi kuliko Imani yetu kwa Mungu. Tusiitumie Sayansi kumtafuta Mungu, bali Mungu atuwezeshe kuijua Sayansi, tena isiyotutoa katika njia sahihi ya wokovu.

Kwa upande mwingine, Thomaso anawakilisha kundi la watu wasioamini Injili inayohubiriwa kila kukicha! Sijui tunataka kumuona Yesu kwa macho?!

Imani huja kwa kusikia, na pasipo Imani hatuwezi kumpendeza Mungu. Yesu alimwambia Thomaso;

Yohana 20:28-29

[28]Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu!
[29]Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.

-Kuna uwezekano Yesu aliwatokea tena wanafunzi ili Thomaso aamini.

Yaani Thomaso alijenga mazingira ya Yesu kuwatokea tena. Yesu hakutaka Thomaso akae bila kuamini.

Thomaso anatufundisha kuwa na hamu, na kiu ya kudumu katika Kristo. Sio kudumu tu, naye aishi ndani yetu, nasi ndani yake.

Thomaso hakuamini kuwa Yesu amefufuka hadi alipomuona. Unasubiri kumuona? Tunapokumbushwa kutembea na Yesu aliyefufuka, fahamu yafuatayo;

i. Yesu mfufuka anatembea na kuishi kati ya watu wake.

ii. Yesu mfufuka anaimarisha imani ya watu wake.

iii. Yesu mfufuka analeta, anao utukufu wa jina lake pitia kwa watu.

Amini Yesu alikufa, na alifufuka kwa ajili yako. Ukimpa maisha yako na kutembea naye siku zote za maisha yako, atakubariki daima na kukupa uzima wa milele. Amina

Tembea na Yesu aliyefufuka.

 

Hii ni Pasaka.

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com