Date: 
03-11-2023
Reading: 
Habakuki 3:1-2

Ijumaa asubuhi 03.11.2023

Habakuki 3:1-2

1 Sala ya nabii Habakuki.

2 Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.

Tutengeneze mambo yaliyoharibika;

Habakuki katika jamii iliyojaa uonevu, udhalimu, kutojali, mateso na kila aina ya unyanyasaji, aliona sala yake haijibiwi;

Habakuki 1:2-3

2 Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.
3 Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.

Baada ya kungojea asione majibu, akaamua kuendelea kusubiri;

Habakuki 2:1

Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.

Baada ya kufahamu kuwa Mungu anajibu kwa wakati wake, sasa Habakuki katika somo la asubuhi hii anaomba Bwana kuifufua kazi yake. Yaani kurejesha upendo, umoja na mshikamano katika jamii ya wakati ule. Alikuwa anamuomba Bwana atengeneze palipoharibika.

Kumbe katika safari yetu ya Imani, tunakumbushwa kufanya yote tukimtazama Kristo ambaye hufanya kwa wakati wake. Tukimkabidhi maisha yetu tutaufurahia uzuri wake kama Habakuki mwenyewe anavyosema;

Habakuki 3:18-19

18 Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.
19 YEHOVA, aliye Bwana, ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.

Ubarikiwe.

Heri Buberwa