Date: 
11-09-2023
Reading: 
Mwanzo 22:15-19

15 Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni
16 akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,
17 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;
18 na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.
19 Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.

Uwakili wetu kwa Bwana

Ibrahimu aliambiwa na Bwana  amtoe sadaka Isaka, mwanae aliyempata uzeeni kwa ahadi toka kwa Mungu mwenyewe. Ibrahimu alitekeleza alichoambiwa na Bwana, yaani alikuwa tayari kumtoa sadaka ya kuteketezwa Isaka. Akiwa tayari kutoa sadaka hiyo, akazuiwa na Bwana;


Mwanzo 22:10-12
10 Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.
11 Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.
12 Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.

Ndipo Ibrahimu akapewa mwanakondoo kwa ajili ya sadaka. Sasa somo letu linaanzia hapo, ambapo Ibrahimu anaahidiwa baraka toka kwa Bwana kwa sababu alikuwa tayari kumtoa mwanae. Anaahidiwa uzao mkubwa mwa sababu ya kuitii sauti ya Bwana.

Ibrahimu alitambua kuwa alipewa Isaka na Bwana, hivyo alikuwa (Isaka) mali ya Bwana. Neno la Mungu linatufundisha kuwa nchi na vyote ni mali ya Bwana kama alivyotambua Ibrahimu;


Zaburi 24:1
Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.

Tunapoanza juma hili tutambue kuwa Mungu ametuumba na kutuweka duniani tumwabudu na kumtumikia, lakini kutunza uumbaji wake. Kwa njia hiyo sisi ni mawakili wake tu. Kwa hiyo tuendelee kuwa mawakili wema, tukitunza uumbaji wake na kumtolea mali alizotupa kwa ajili ya kazi yake. Tambua kuwa vitu vyote ulivyo navyo ni mali yake, hivyo uwe wakili mwema wa Bwana. Amina.


Tunakutakia wiki njema yenye  uwakili mwema.

-----------------------------------------

Heri Buberwa 
Mlutheri