Jumamosi asubuhi tarehe 29.07.2023
2 Wafalme 8:1-6
1 Basi Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke, ambaye alimfufulia mwanawe, akasema, Ondoka, ukaende wewe na jamaa yako, ukae hali ya kigeni utakakoweza kukaa; kwa sababu Bwana ameiita njaa; nayo itakuja juu ya nchi hii muda wa miaka saba.
2 Akaondoka yule mwanamke, akafanya kama alivyosema mtu wa Mungu; akaenda, yeye na jamaa yake, akakaa katika nchi ya Wafilisti miaka saba.
3 Ikawa miaka saba ilipoisha, yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti; akatokea amlilie mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.
4 Basi mfalme alikuwa akizungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, akinena, Uniambie, nakusihi, mambo makuu yote aliyoyafanya Elisha.
5 Ikawa, alipokuwa katika kumwambia mfalme jinsi alivyomfufua mtu aliyekufa, tazama, huyo mwanamke aliyemfufulia mwanawe, alimlilia mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake. Gehazi akasema, Bwana wangu mfalme, huyu ndiye mwanamke, na huyu ndiye mwanawe, ambaye Elisha alimfufua.
6 Na mfalme alipomwuliza yule mwanamke, yeye akamweleza. Basi mfalme akamtolea akida, akasema, Mrudishie yote aliyokuwa nayo, na mapato yote ya shamba lake tangu siku aliposafiri, hata leo.
Uchaguzi wa busara;
Ukisoma sura ya nne, unaona jinsi Nabii Elisha alivyomfufua kwa msaada wa Bwana mtoto aliyekufa. Mama wa yule mtoto alikuwa akimtunza Elisha katika huduma yake. Sasa katika sura ya 8 Elisha anamuelekeza mwanamke yule kuelekea nchi ya kigeni kwa sababu ya njaa iliyokuwa inakaribia.
Mwanamke aliondoka na baada ya miaka saba alirudi akamlilia mfalme kwa ajili ya mali zake alizokuwa ameziacha alipoondoka, akarudishiwa mali zake. Mwanamke alirudishiwa mali zake kwa kuwa mtii kwa Nabii Elisha toka wakati ule akimtunza katika huduma, akamsikiliza alipomwambia kuondoka na kwenda uhamishoni.
Lakini pia mwanamke alikuwa mtii kwa Mfalme aliporudi toka uhamishoni, alipomlikia akamrudishia mali zake.
Utii ulimsaidia katika maisha yake.
Tukimtii Kristo tunachagua kwa busara. Jumamosi njema.
Heri B.