Katika ibada ya Alhamisi Kuu iliyofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, 6 Aprili 2023 na kuongozwa na Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa iliwakutanisha washarika na wageni mbalimbali kukumbuka siku ambayo Yesu Kristo alisalitiwa na mmoja wa wanafunzi wake aliyejulikana kama Yuda Iskarioti na hivyo kupelekea kukamatwa, kuteswa na kufa kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Akizungumza katika utangulizi wa ibada hiyo Baba Askofu alisema kuwa Ijumaa Kuu ni siku ambayo Mwokozi Yesu Kristo alianzisha utamaduni wa Chakula cha Bwana kama alama ya upendo kwetu sisi tulio watoto wake pamoja na kwa kanisa. Pia hii ni siku ambayo uhasi ulianza na kujihiridhisha. “Tungekuwa na siku kama kimataifa wanavyoweka, basi tungesema kuwa leo ni siku ya wasaliti”, Baba Askofu alidokeza.
Somo: Mwili Na Damu Ya Yesu Kwa Uzima wa Milele; Yohana 6: 52 - 59
52 Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? 53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. 54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. 55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. 57 Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. 58 Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele. 59 Maneno hayo aliyasema katika sinagogi, alipokuwa akifundisha, huko Kapernaumu.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo Baba Askofu Dkt. Malasusa aliwakumbusha wakristo kujihoji na kujitafakari wanaposogea na kushiriki katika meza ya Bwana. “Inapotangazwa Jumapili ijayo tutashiriki meza ya Bwana maana yake ni watu wajihoji na kujitengeneza wenyewe, na pale unapoona kwamba yamekushinda, nenda kwa mchungaji. Ndugu zangu naomba leo nikumbushe, haijalishi mara ngapi unashiriki meza ya Bwana kwa mwaka lakini mara ngapi umeshiriki kihalisia kwamba kweli unampokea Yesu, unapokea mwili wake na damu yake. Haijalishi mara ngapi umeshiriki ibada, lakini je, uhusiano wako na Mungu ukoje?” alisema Baba Askofu.
“Damu yake iliyomwagika pale msalabani ndiyo iliyotuokoa, hivyo tunapoenda kushiriki meza ya Bwana naomba nikwambie kwamba kwenye damu ya Yesu kuna nguvu ya ajabu. Hakuna kitu chochote kilicho hai kisichotegemea damu. Mwanadamu hawezi kukufutia dhambi bali damu ya Yesu ndiyo inayofuta dhambi,” aliongeza Baba Askofu.
Dean Chediel Lwiza na Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Azania Front Chaplain Charles Mzinga ni miongoni wa watumishi waliohuduria ibada hiyo ambayo iliambatana na Chakula cha Bwana.Aidha Mchungaji Joseph Mlaki aliongoza Ibada ya Kiingereza.
PICHA KUTOKA KWENYE IBADA;
Kutazama Ibada za Alhamisi Kuu:
Ibada ya Kiingereza: https://www.youtube.com/watch?v=WHuCY_Uw6xc
Ibada ya Kiswahili: https://www.youtube.com/watch?v=GWc6tfcf8Jk&t=1673s