Date: 
15-02-2022
Reading: 
Mwanzo 41:28-36

Jumanne asubuhi tarehe 15.02.2022

Mwanzo 41:28-36

28 Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.

29 Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.

30 Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi.

31 Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana.

32 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.

33 Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri.

34 Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba.

35 Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji.

36 Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.

Tunaokolewa kwa neema;

Yusufu anatafsiri ndoto aliyoota Farao kuwa itakuja miaka saba ya shibe na miaka saba ya njaa. Farao alimpenda Yusufu na kumfanya mtawala anayefuatia chini yake. Ni kwa sababu wengi walishindwa kutafsiri ile ndoto.

Kumbuka Yusufu alikuwa mtumwa kwenye himaya ya mfalme. Kwa neema anakuwa mtawala wa Misri akimsaidia mfalme! Mungu alimtumia Yusufu kuinusuru nchi na njaa kwa miaka saba kupitia kwa Yusufu! Yaani Mungu aliwapatia chakula wakati wa njaa kali! Bila shaka ni neema ya Mungu.

Tutambue kuwa nafasi ya Mungu iko palepale, kuwa yeye ndiye ngao yetu wakati wote. Tusichoke kuliita jina lake, maana yeye hutujalia neema yake siku zote.

Siku njema.