Date: 
20-12-2022
Reading: 
Luka 7:24-26

Hii ni Advent 

Jumanne asubuhi tarehe 20.12.2022

Luka 7:24-26

[24]Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo?

[25]Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme.

[26]Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii.

Bwana yu karibu;

Yohana alikuwa amefungwa gerezani na Herode, akawatuma wanafunzi wake kwa Yesu kumuuliza kama yeye ndiye Mesiya. Yesu akawapa ujumbe kwamba ni yeye. Ndipo linakuja somo la asubuhi hii, kwamba wanafunzi wa Yohana walipoondoka, Yesu akaanza kuwasimulia habari za Yohana. Anawauliza walifuata nini jangwani? Kwa maana nyingine anawauliza walimuonaje? Ujumbe waliupokea?

Ukiendelea kusoma mbele baada ya somo la asubuhi hii unaona Yesu akiwaambia makutano kwamba yule ni Yohana aliyeleta habari njema, kwamba Mwokozi atakuja hivyo watu watengeneze maisha yao kumpokea;

Luka 7:27-28

[27]Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, 
Tazama, namtuma mjumbe wangu 
Mbele ya uso wako, 
Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.

[28]Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.

Katika mstari wa 28 Yesu anathibitisha kuwa yeye ni mkuu kuliko Yohana. Hii ni kweli, maana Yohana alimtangulia Yesu akitangaza ujio wake, lakini Yesu ndiye alikuja kuokoa wanadamu na dhambi zao. Yesu huyu ndiye tunayemngojea kurudi tena kulichukua Kanisa. Andaa moyo wako maana Bwana yu karibu. 

Jumanne njema.