Date: 
12-12-2022
Reading: 
Isaya 40:1-5

Hii ni Advent;

Jumatatu asubuhi tarehe 12.12.2022

Isaya 40:1-5

[1]Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu, asema Mungu wenu.

[2]Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa BWANA adhabu maradufu kwa dhambi zake zote.

[3]Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, 

Itengenezeni nyikani njia ya BWANA; 

Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.

[4]Kila bonde litainuliwa, 

Na kila mlima na kilima kitashushwa; 

Palipopotoka patakuwa pamenyoka, 

Na palipoparuza patasawazishwa;

[5]Na utukufu wa BWANA utafunuliwa, 

Na wote wenye mwili watauona pamoja; 

Kwa kuwa kinywa cha BWANA kimenena haya.

Bwana anawafariji watu wake;

Bwana Asifiwe;

Somo la asubuhi hii ni unabii wa Isaya kuhusu ukombozi wa Israeli, uliotolewa wakati Israeli wakiwa uhamishoni Babeli. Isaya anarudia maneno "watulizeni mioyo" kukazia ukombozi wa Israeli. Katika ukombozi huo, Isaya anatabiri ujio wa aliyemtangulia mkombozi pale anaposema "sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, itengenezeni nyikani njia ya Bwana..."

Agano jipya huthibitisha kuwa aliyetabiriwa na Isaya ni Yohana Mbatizaji;

Mathayo 3:1-3

[1]Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema,
[2]Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
[3]Kwa sababu huyo ndiye aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, 
Sauti ya mtu aliaye nyikani, 
Itengenezeni njia ya Bwana, 
Yanyosheni mapito yake.

Hivyo, Israeli wakiwa uhamishoni walipewa habari ya kukombolewa kwao. Ukombozi wao ilikuwa ni zaidi ya kutoka uhamishoni. Taifa la Israeli liliahidiwa ukombozi ambao ungeletwa na Yesu Kristo, ambaye alitambulishwa na Yohana Mbatizaji.

Ujumbe ya Yohana ulikuwa kutengeneza mapito ya Bwana, yaani kuandaa mioyo ili kumpokea Kristo ambaye alikuja kuwakomboa Israeli.

Tumpokee Yesu mioyoni mwetu akae kwetu maana yeye ndiye mfariji wetu, tukijiandaa na kurudi kwake kwa mara ya pili

Uwe na wiki njema yenye ushuhuda

Amina.