Date: 
12-09-2022
Reading: 
Habakuki 2:12-15

Jumatatu asubuhi tarehe 12.09.2022

Habakuki 2:12-15

[12]Ole wake yeye ajengaye mji kwa damu, awekaye imara mji mkubwa kwa uovu!

[13]Angalieni; je! Jambo hili halikutoka kwa BWANA wa majeshi, kwamba watu wajishughulikie moto, na mataifa wajisumbue kwa ajili ya ubatili?

[14]Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa BWANA, kama maji yaifunikavyo bahari.

[15]Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia, ili kuutazama uchi wao!

Jirani yako ni nani?

Nabii Habakuki alimlalamikia Bwana kwa kunyamaza katikati ya uovu uliokuwa umekithiri. Hapakuwa na haki. Wanyonge walionewa sana. Mungu alimjibu Habakuki, kuwa watu watende haki, maana Imani ya kweli msingi wake ni kutenda haki. 

Somo la asubuhi hii ni maelekezo ya Habakuki toka kwa Bwana, kwamba waovu watapata dhiki. Waovu ni wale waliwaonea wengine, ambao Bwana aliwataka kutenda haki. Mstari wa 15 unatoa ole kwake ampaye kileo jirani yake ili kumuaibisha. Naweza kusema hii ni ole kwake amtendeaye mabaya jirani yake.

Habakuki anatupa ujumbe wa kutenda haki katika jamii yetu. Mazingira ya wakati wa Habakuki hayana tofauti na sasa. Tupo baadhi yetu tunaowafanyia ubaya wenzetu. Hawa machozi yao hayawezi kwenda bure ukizingatia hawana hatia. Ujumbe wa Habakuki ni kuwa ipo dhiki kwa waovu, wale wawatendeao jirani zao ubaya. Tuwatendee mema jirani zetu, ndivyo Mungu anavyotaka.

Uwe na wiki njema, wewe na jirani zako.